Sunday, April 27, 2025

Tanzania Yaondoa Zuio la Bidhaa za Kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi



Serikali ya Tanzania imeondoa rasmi zuio la kuingiza bidhaa za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi, hatua inayolenga kutoa nafasi kwa majadiliano ya kidiplomasia na kiutaalamu kati ya pande hizo tatu.

Zuio hilo lilitangazwa awali na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kupitia mitandao ya kijamii, ambapo alieleza kuwa kuanzia Aprili 17, 2025, Tanzania ingezuia uingizaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini. Hata hivyo, baada ya siku mbili za utekelezaji, serikali imeamua kuliondoa.

Kupitia taarifa rasmi ya Wizara ya Kilimo iliyotolewa Aprili 25, 2025 na kusainiwa na Bashe, imeelezwa kuwa:
"Kwa misingi hiyo, Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Aprili 26, 2025 tukiamini majadiliano yanayoendelea yataleta suluhisho."

Bashe amesema kuwa kutokana na zuio hilo, Serikali za Malawi na Afrika Kusini ziliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo ya Tanzania, kwa lengo la kutafuta njia ya pamoja ya kushughulikia changamoto zilizojitokeza.

"Makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Serikali ya Malawi itatuma ujumbe wake Mei 2, 2025, utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje akiambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo ili kukutana na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma," amesema Bashe.

Kuhusu Afrika Kusini, amesema kuwa mazungumzo yanaendelea baina ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na mamlaka husika kutoka Afrika Kusini zinazoshughulikia masuala ya afya ya mimea na masoko.

Bashe amesisitiza kuwa serikali itaendelea kulinda maslahi ya wakulima na wananchi wa Tanzania, huku ikiheshimu misingi ya biashara huria na mahusiano ya kimataifa.

"Serikali inawahakikishia wakulima na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kuwa, uhuru wa biashara ya mazao ya kilimo utaendelea kwa kuzingatia matakwa ya afya ya mimea, usalama wa rasilimali za nchi na uhusiano wa kidiplomasia kwa manufaa ya wote," amesema.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Tanzania katika kutafuta suluhisho la amani kupitia mashauriano, bila kuathiri usalama wa kilimo na maslahi ya taifa.

No comments:

Post a Comment