Dereva wa basi la Kampuni ya Mvungi, Al-Adani Mruma (47), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi akikabiliwa na mashtaka 29, likiwemo la kusababisha vifo vya watu saba na kuwajeruhi wengine 42, kufuatia ajali iliyotokea tarehe 3 Aprili 2025 katika Kijiji cha Mamba, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12:45 asubuhi, wakati basi hilo aina ya Yutong lenye namba za usajili T 222 DNL, lilipokuwa likitokea Ugweno kuelekea Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa ajali ilisababishwa na uzembe wa dereva, baada ya kushindwa kulimudu gari alipokuwa akipishana na gari jingine kwenye kona kali, hali iliyosababisha basi hilo kutoka barabarani na kutumbukia bondeni.
Mruma alifikishwa mahakamani tarehe 23 Aprili 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Ally Mkama, ambapo alisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Julieth Komba, anayesaidiana na Bertina Tarimo.
Wakili Komba alisema: “Mshtakiwa alitenda makosa hayo tarehe 3 Aprili 2025 katika barabara ya Ugweno, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, akiwa dereva wa basi la abiria.”
Mashtaka yanayomkabili Mruma ni pamoja na kusababisha vifo kwa uzembe, kuharibu mali na kusababisha majeraha kwa abiria waliokuwemo ndani ya basi hilo.
Hata hivyo, Mruma amekana mashtaka yote yaliyosomwa dhidi yake. Shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kisheria, huku mshtakiwa akiendelea kushikiliwa.

No comments:
Post a Comment