Dar es Salaam, Aprili 25, 2025 — Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hilda Newton, ameachiwa kwa dhamana leo saa moja jioni katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati (Central Police Station), jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Hilda, Jebra Kambole, amethibitisha kuachiwa kwa mteja wake mbele ya waandishi wa habari, akisema:
“Hilda Newton ameachiwa kwa dhamana, lakini atatakiwa kuripoti katika kituo hiki cha polisi cha Kati kila Jumatano.”
Kabla ya kuachiwa kwake, kulikuwepo hali ya sintofahamu kuhusu mahali alikokuwa Hilda tangu alivyokamatwa siku ya jana akiwa katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Chama chake, CHADEMA, kilieleza kutokuwa na taarifa rasmi kuhusu aliko mwanachama wao huyo.
Akizungumza mapema leo na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Amani Golugwa, alisema:
“Tuna mwanachama wetu ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu, Bi. Hilda Newton. Kama ofisi zetu za chama, hatuna taarifa zozote zilizo rasmi zinazoonyesha kwamba Hilda Newton yuko wapi.”
Golugwa alieleza kuwa Hilda alikamatwa jana eneo la Kisutu, na chama kilitarajia jina lake litatajwa katika taarifa ya polisi iliyotolewa jana.
“Jana kwenye taarifa ambayo Afande Muliro alitaja majina ya viongozi na wanachama ambao wapo kwenye mikono ya Jeshi la Polisi, jina la Hilda halikutajwa.
Pia alitoa taarifa kuhusiana na mtu mmoja aliyeokotwa kwenye ufukwe wa Coco Beach, lakini taarifa ya Hilda Newton kuwa kwenye mikono ya polisi haikutolewa,” alisema Golugwa.
Mpaka sasa, sababu rasmi ya kukamatwa kwa Hilda Newton haijawekwa wazi na Jeshi la Polisi, huku wakili wake na chama wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za kikatiba za raia na kutoa taarifa kwa uwazi kuhusu watu walioko mikononi mwa vyombo vya dola.


No comments:
Post a Comment