Friday, April 25, 2025

Dkt. Biteko Aridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Utawala TICD



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ameelezea kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la utawala katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD).



Akizungumza leo, Aprili 25, 2025, wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi huo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha, Dkt. Biteko amesema amefurahishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa kwa ubora na kwa kuzingatia viwango.



"Nimekagua mradi huu na kuona mmeanza vizuri. Nina imani mtaukamilisha kwa mafanikio makubwa. Nawapongeza kwa usimamizi mzuri," amesema Dkt. Biteko.



Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt. Bakari George, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.6 hadi kukamilika kwake.


Ameeleza kuwa jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu na sakafu nne, likijumuisha ofisi 44 na kumbi tano za mikutano zitakazoweza kuchukua jumla ya watu 545 kwa wakati mmoja.

"Jengo hili litakuwa la kisasa, likiwa na mifumo yote muhimu ikiwemo mfumo wa umeme, mfumo wa kuzuia majanga ya moto, mfumo wa TEHAMA, mfumo wa kiyoyozi, pamoja na mfumo wa maji safi na maji taka," amesema Dkt. Bakari.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema Wizara itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutumika kwa manufaa ya chuo na taifa kwa ujumla.

"Wizara itaendelea kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya TICD," amesema Dkt. Jingu.

No comments:

Post a Comment