Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesisitiza kuwa chama chake hakibishani na CHADEMA ila hakiko tayari kupoteza muda katika majadiliano yasiyozaa matunda.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Wasira alijibu kauli za Zitto Kabwe na viongozi wa CHADEMA, akisema kuwa CCM tayari imeonyesha wazi kuwa kama kuna majadiliano ya maana, basi yatafanyika, lakini hawatashiriki katika majadiliano yasiyoleta matokeo.
Alisema kuwa CCM kimewahi kusema kwa wazi kuwa kama CHADEMA wana jambo la kujadili, basi waje na hoja zinazoweza kujadiliwa. Wasira aliongeza kuwa chama hicho kinataka kujua ni mabadiliko gani CHADEMA wanayotaka na kusema kuwa hadi sasa hawajatoa maelezo ya kina kuhusu mabadiliko wanayodai.
Wasira alikashifu kauli ya Zitto Kabwe aliyesema kuwa CCM imekataa mazungumzo na CHADEMA, akisisitiza kuwa CCM ni mwanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ambacho kinahusisha vyama vyote vya siasa, na kwamba chama chake hakijakataaa kuzungumza na Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA.
Alisema kuwa CCM iko tayari kushiriki katika mazungumzo yoyote ya amani, na hata maandamano kama yataitishwa, chama chake kitashiriki ili kudumisha amani na demokrasia.
Pia, Wasira alieleza kuwa wanachama wa CHADEMA wameanza kuwageuka viongozi wao, na hivyo ni muhimu kwao kuwa wazi na kusema ni nini hasa wanataka kutoka kwa serikali na kwa wananchi wa Tanzania. Alisema kuwa CCM imefanya mageuzi makubwa katika utawala wake, na sasa ni wakati wa CHADEMA kueleza mabadiliko wanayotaka kwa uwazi.


0 Comments:
Post a Comment