"Kuanzia Sasa Wachoma Nyama Watatumia Nishati Safi" – Makonda

 


 

Arusha, Tanzania – Serikali ya Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati imetoa majiko ya nishati safi kwa wachoma nyama wa mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuondokana na matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni. Hatua hii inalenga kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji miti hovyo.



Akizungumza leo Machi 07, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda ametangaza kuwa wachoma nyama wote wa mkoa huo watawekewa mpango wa kupata majiko mbadala ya nishati safi. 



"Kuanzia sasa, shughuli zote za uchomaji nyama Mkoani Arusha zitatumia nishati safi. Tunataka kulinda afya za wananchi wetu na mazingira yetu," alisema Makonda.



Kwa upande wake, baadhi ya wachoma nyama walioanza kutumia nishati safi walieleza tofauti kubwa kati ya nishati hiyo na mkaa. 



Walisema kuwa majiko hayo mapya yanapunguza moshi na yanawapatia faida zaidi kiuchumi.



Makonda aliongeza kuwa wananchi watakaohudhuria hafla ya Nyama Choma jioni ya leo watapata fursa ya kuonja nyama zilizochomwa kwa kutumia nishati safi, akisisitiza kuwa juhudi hizi zinaungwa mkono na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 



"Tunapenda wananchi waje waonje ladha ya nyama iliyopikwa kwa nishati safi. Huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa kwenye sekta ya chakula na mazingira," alisisitiza.



Hatua hii inakuja wakati serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama njia ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda afya za wananchi.



0 Comments:

Post a Comment