Mahakama Kuu ya Uganda imewaamuru maafisa wa gereza kumrudisha gerezani kiongozi wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, licha ya hali yake ya afya kuendelea kudhoofika.
Besigye, ambaye amekuwa kwenye mgomo wa kususia chakula kwa zaidi ya wiki moja, anazidi kuzorota kiafya hali inayoongeza hofu kwa familia yake na mawakili wake.
"Nimeumia lakini sijashtuka"
Baada ya uamuzi huo wa mahakama, mke wa Besigye, Winnie Byanyima, alieleza masikitiko yake mbele ya waandishi wa habari.
"Nilikuja hapa nikitarajia kuondoka na Dk. Kizza Besigye kwenda naye nyumbani leo, nimeumia lakini sijashtuka. Besigye ni mateka, alitekwa nyara," alisema Byanyima.
Besigye na mshitakiwa mwenzake, Hajji Obeid Lutale, walifikishwa mahakamani jijini Kampala kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi lao la kutaka kuachiliwa.
Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa Besigye ni mgonjwa na hakuweza kuendelea na kesi, hivyo kuamuru arejeshwe gerezani, ambako amekuwa akishikiliwa kwa takriban miezi minne.
Kukamatwa katika mazingira tata
Besigye, aliyewahi kuwa daktari binafsi wa Rais Yoweri Museveni, alikamatwa Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale.
Baadaye walifikishwa katika mahakama ya kijeshi jijini Kampala na kushtakiwa kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria – madai ambayo wamekanusha vikali.
Katika uamuzi wa kihistoria mwezi uliopita, Mahakama ya Juu Zaidi nchini Uganda ilitangaza kuwa ni kinyume cha katiba kwa mahakama za kijeshi kusikiliza kesi za kiraia, na kuamuru kesi hiyo ihamishiwe mahakama za kiraia.
Uamuzi huo ulimkasirisha Rais Museveni, ambaye alieleza wazi kutoridhishwa kwake na hukumu hiyo.
"Uamuzi mbaya wa mahakama"
Katika ujumbe wake mrefu kwenye mtandao wa X, Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa takriban miongo minne, aliikosoa mahakama kwa "kuchelewesha kesi ya Besigye kufuatia uamuzi wake."
Makataa ya saa 48 kutoka kwa upinzani
Wakati huohuo, wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na nyota wa zamani wa muziki wa pop, Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine, wanapanga kufanya kikao cha pamoja cha maombi kwa ajili ya Besigye na wafungwa wengine wa kisiasa.
Katika mkutano wao na waandishi wa habari Jumatatu jioni, viongozi wa upinzani walitoa makataa ya saa 48 kwa serikali kumwachilia Besigye na wafungwa wote wa kisiasa.
Je, serikali ya Uganda itasikiliza kilio cha familia, wafuasi wa Besigye na wanasiasa wa upinzani? Ama itaendelea kushikilia msimamo wake wa kumuweka gerezani licha ya afya yake kuendelea kuzorota?
0 Comments:
Post a Comment