Tuesday, January 7, 2025

POLISI YAPOKEA VIFAA VYA KUPIMA MADEREVA WANAOENDESHA VYOMBO VYA MOTO WAKIWA WAMEKUNYWA POMBE




Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura amesema Jeshi la Polisi limeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ajali za barabarani ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyokuwa akiyatoa mara kwa mara ya kuhakikisha ajali za barabarani zinadhibitiwa ipasavyo.



IGP Wambura ameyasema hayo wakati akipokea vifaa 3050 kati ya 10000 vya kupima ulevi kwa madereva kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) vilivyokabidhiwa na Mkurugenzi wa LATRA, CPA Habibu Saluo, Makao Makuu ya Polisi Jijini Dodoma Januari 6, 2025.


IGP Wambura alisema kupitia Kikosi cha Usalama barabarani watakuwa wakali kwa madereva wazembe ambao wamekuwa wakisababisha ajali za barabarani ambapo pia wataendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kuwa watanzania wanakuwa salama.


"Tumeweza kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali na sasa nguvu pia tunazielekeza kwenye usalama barabarani kwa kuwa takwimu za ajali bado zipo juu hivyo ni lazima tuwe wakali sana ili kuona sheria za usalama barabarani zinafuatwa ili kuokoa maisha ya watanzania," alisema IGP Wambura.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amesema, utendaji kazi wao unahitaji sana ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kusimamia Sheria za Usalama Barabarani na hivyo vipima ulevi hivyo vitasaidia Kikosi cha Usalama Barabarani katika kudhibiti ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva walevi na wazembe pindi wanapokuwa barabarani na kuendesha pasipo kuzingatia sheria.


CPA Suluo alisema uwepo wa vifaa hivyo utasaidia kupima madereva mara kwa mara wawapo barabarani jambo ambalo litasaidia kufanya barabara zetu kuwa salama.


Aidha alisema wataendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo matumizi ya mifumo katika kufanya ukaguzi wa magari ambapo kwa sasa wanaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali.


Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo ilihudhuriwa na Makamishna wa Polisi, Manaibu Kamishna wa Polisi, baadhi ya Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi na Maofisa kutoka LATRA.

No comments:

Post a Comment