Friday, January 10, 2025

Makonda Aagiza Ujenzi wa Jengo la Utawala Jiji la Arusha Ukamilike Mei

  

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, leo Alhamisi Januari 09, 2025, ametoa maagizo  kwa mkandarasi anayesimamia ujenzi  wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.



Makonda amemuagiza mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika ifikapo Mei 2025, badala ya Julai kama ilivyokuwa imepangwa awali.



Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo,  Makonda alisema, "Mradi huu umeonekana kusuasua bila sababu za msingi, ilhali Rais Samia Suluhu Hassan tayari alishatenga zaidi ya bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya pili ya jengo hili lenye ghorofa sita."



Aliendelea kusema kuwa, “Lazima kumaliza kazi kwa wakati. Hatuwezi kukubali mradi huu uchelewe, kwa sababu serikali ya Rais Samia inatoa fedha, lakini miradi inakuwa haikamiliki kwa wakati."


Aidha, Makonda alisisitiza kuwa, “Taratibu za kimkataba na ujenzi kwa awamu ya tatu zinapaswa kuanza kuandaliwa mara moja, badala ya kusubiri awamu ya pili kukamilika."


Katika hatua nyingine, Makonda aliagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanawapa kipaumbele wenyeji wa Arusha na watu wenye sifa kwenye tenda mbalimbali. Lengo ni kukuza uchumi wa mkoa na kuhakikisha manufaa yanawafaidi wananchi.


“Viongozi na Madiwani wa Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha, hakikisheni kila kitu mnachofanya kinakuwa na matokeo chanya kwa wananchi. Tunapaswa kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi, kama sehemu ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha maendeleo na ustawi wa wananchi wake," aliongeza Mhe. Makonda.



Kwa upande wao, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Mhe. Maximilian Iranghe, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa, walimshukuru Mhe. Makonda kwa juhudi zake katika kukuza uwajibikaji Mkoani Arusha. Walisema kuwa wataendelea kushirikiana na wataalamu na watendaji wengine kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Makonda unafanyika haraka na kwa ufanisi ili wananchi wanufaike na ujenzi wa jengo hilo.

"Kwa pamoja tutashirikiana kuhakikisha ujenzi huu unakamilika kwa wakati, ili wananchi wetu wafaidike na maendeleo haya," alisema Mhe. Iranghe.

No comments:

Post a Comment