Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kampuni ya utalii ya Leopard Tours, na Mtume Boniface Mwamposa wa Kanisa la Arise and Shine wamekabidhi pikipiki 60 kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha.
Hatua hii inalenga kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii katika mkoa huo.
Pikipiki hizo 20 zimetolewa na NSSF, 20 kutoka Leopard Tours, na nyingine 20 kutoka kwa Mtume Mwamposa.
Hafla ya kukabidhi msaada ilifanyika leo, Desemba 18, 2024 kwenye viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, na kuhudhuriwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Justine Masejo, pamoja na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, meya wa jiji la Arusha, na wenyeviti wa halmashauri za mkoa wa Arusha.
Utoaji wa Msaada na Umuhimu wake kwa NSSF na Jamii
Lulu Mengele, Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), alieleza kwa kina sababu za kushiriki katika kuchangia pikipiki kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Mengele alisema msaada huo ni sehemu ya kujibu ombi lililowasilishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, likiwa na lengo la kuboresha ufanisi wa jeshi la polisi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao.
"Tulipokea ombi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, na baada ya kulichambua, tuliona ni muhimu sana kwetu NSSF kushiriki katika kuchangia vifaa hivi vya usafiri.
Jeshi la polisi lina jukumu kubwa la kulinda raia na mali zao, na hili lina mchango wa moja kwa moja katika kuimarisha amani na mazingira ya uwekezaji na biashara, hasa kwenye sekta ya utalii ambayo ni muhimu kwa mkoa huu wa Arusha," alisema Mengele.
Mengele alifafanua kuwa NSSF, kama mfuko wa hifadhi ya jamii, unao wajibu wa kuunga mkono juhudi za maendeleo ambazo kwa namna moja au nyingine zina mchango wa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya wananchi.
Alieleza kuwa msaada huo wa pikipiki ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa mazingira ya kiusalama yanaboreshwa, jambo linalosaidia sekta ya utalii kuimarika na pia kuleta fursa za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.
"Pikipiki hizi zitaimarisha uwezo wa jeshi la polisi kufanya doria na kushughulikia changamoto za kiusalama kwa haraka zaidi. Hii itasaidia si tu kuimarisha usalama wa raia na mali zao, bali pia kuifanya Arusha kuwa mahali salama kwa wageni, wawekezaji, na watalii.
Kwa upande wetu kama NSSF, tunatambua kuwa mazingira mazuri ya kiusalama yana mchango mkubwa katika kuhakikisha wanachama wetu wanaendelea kunufaika na huduma zetu," aliongeza.
Alieleza kuwa msaada huo pia unalenga kuongeza mwamko kwa wananchi kujiunga na NSSF, akisema, "Tunataka kuhakikisha kuwa kila mwananchi mwenye kipato anaweza kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii.
Lengo letu ni kuwalinda wanachama wetu si tu katika ajali za kazi, bali pia katika maisha yao ya kila siku. Kupitia mchango wa mwanachama mmoja wa Shilingi 30,000 kwa mwezi, au Shilingi 52,000 kwa familia, tunawawezesha wanachama kupata huduma za matibabu popote wanapohitaji."
"Leo tumepokea msaada wa pikipiki 60; 20 kutoka NSSF, 20 kutoka Leopard Tours, na 20 kutoka kwa Mtume Mwamposa. Wadau hawa hawakuombwa, bali wameguswa na umuhimu wa kuchangia maendeleo ya mkoa wetu," alisema Makonda.
Aliongeza kuwa mkoa huo unaendelea kuvunja rekodi kwa kusajili wanachama wapya wa NSSF kutoka taasisi rasmi na zisizo rasmi, akiwataka wakuu wa wilaya kuhakikisha kila wilaya inasajili wanachama 10,000 ndani ya miezi mitatu kupitia mpango uliopo.
"Pikipiki hizi zitasaidia kuimarisha doria na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuhakikisha wananchi na mali zao zinalindwa kwa usalama wa hali ya juu," alisema Masejo.
Mtume Boniface Mwamposa, kwa upande wake, aliahidi kuendelea kujitoa kwa maendeleo ya mkoa wa Arusha, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuchangia ustawi wa jamii.
Msaada huo wa pikipiki unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu katika kuhakikisha mkoa wa Arusha unakuwa salama na kivutio kwa watalii, wafanyabiashara, na wageni wanaofika kwa shughuli mbalimbali.
0 Comments:
Post a Comment