Wednesday, December 4, 2024

NCAA Yazindua Kampeni ya Utalii wa Ndani “Merry and Wild; Ngorongoro Awaits”

 


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) leo imezindua kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani msimu wa sikukuu, yenye kauli mbiu “Merry and Wild; Ngorongoro Awaits.” Kampeni hii inalenga kuwawezesha Watanzania kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kufurahia vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika eneo hilo la urithi wa dunia.  



Akizungumza na vyombo vya habari jijini Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Utalii na Masoko wa NCAA, Mariam Kobelo, alisema kampeni hiyo itaanza leo tarehe 4 Desemba 2024 na kumalizika tarehe 4 Januari 2025.  


"Kampeni hii imelenga kuhamasisha Watanzania wengi zaidi kutembelea maeneo ya hifadhi, kujionea vivutio vyetu vya kipekee na kufurahia sikukuu kwa namna ya kipekee. 


Tumeandaa vifurushi maalum kwa gharama nafuu, tukishirikiana na kampuni ya Smile Safaris,” alisema Kobelo.  

Vifurushi Vilivyotangazwa  

Kampeni hii imetangaza vifurushi vitatu vinavyolenga kuwarahisishia Watanzania kufanya utalii:  


1. Kifurushi cha Faru 

   - Gharama: Shilingi 450,000 kwa kila mtu  

   - Huduma: Utalii wa siku mbili (tarehe 24-25 Desemba 2024), kiingilio, malazi, chakula, muongoza watalii, usafiri na huduma ya picha.  


2. Kifurushi cha Tembo 

   - Gharama: Shilingi 130,000 kwa kila mtu  

   - Huduma: Utalii wa siku moja (Day Trip), kiingilio, chakula, muongoza watalii, usafiri na huduma ya picha.  


3Kifurushi cha Chui

   - Gharama: Shilingi 85,000 kwa kila mtu  

   - Huduma: Utalii wa siku moja (Day Trip), usafiri wa basi, kiingilio, chakula, muongoza watalii na huduma ya picha.  



Kwa mujibu wa Kobelo, vivutio vitakavyotembelewa ni pamoja na urithi wa utamaduni Olduvai, Kreta ya Empakai na Olmoti, Mlima Lormolasi, na pia msimu wa Ndutu ambapo nyumbu wengi hujifungua kabla ya kuanza safari zao kuelekea Maasai Mara, Kenya.  


Hamasa Kupitia Vijana wa Action Rollers Skates


Kobelo aliongeza kuwa kampeni hii itahamasishwa pia kupitia vijana maalum wa 'Action Rollers Skates' ambao watatembelea mitaa mbalimbali ya Arusha, Dar es Salaam, na Zanzibar kati ya tarehe 4 na 16 Desemba 2024.  



Mkoa wa Arusha Watoa Msimamo 


Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji Mali, Daniel Loiruki, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, alisema kampeni hii ni muhimu katika kuongeza hamasa ya Watanzania kutembelea vivutio vya utalii.  


“Mpango wa kuboresha sekta ya utalii mkoani Arusha upo mbioni. Tunaunga mkono jitihada za NCAA za kuhamasisha Watanzania kupenda na kutembelea vivutio vyetu vya kipekee," alisema Loiruki.  



Ukuaji wa Utalii wa Ndani 

Kobelo alibainisha kuwa idadi ya Watanzania wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka, ambapo zaidi ya watalii 200,000 wa ndani walitembelea hifadhi hiyo kati ya Julai na Novemba 2024. Hata hivyo, alisema bado kuna fursa kubwa ya kukuza idadi hiyo kupitia kampeni kama hii.  


“Kupitia kampeni hii, tunataka kuhakikisha kila Mtanzania ana fursa ya kufurahia vivutio vya kipekee vilivyopo katika hifadhi zetu,” aliongeza.  


Watanzania wanahimizwa kuchagua vifurushi vinavyowafaa kwa kupiga namba ya simu 0755 559013 ili kuweka nafasi zao na kupata maelezo zaidi kupitia kampuni ya Smile Safaris.

No comments:

Post a Comment