Monday, October 7, 2024

Mama Yake Sean "Diddy" Combs Asema "Amesikitishwa" na Tuhuma Dhidi ya Mwanaye

 



Mama wa mwanamuziki maarufu Sean "Diddy" Combs, Janice Small Combs, amesema kuwa "amesikitishwa na kuhuzunishwa sana" na tuhuma zinazotolewa dhidi ya mwanaye, akizitaja kuwa ni za "uongo." 



Sean Combs, anayejulikana kwa nyimbo maarufu kama "I'll Be Missing You" ya mwaka 1997, alikamatwa mwezi uliopita kwa tuhuma za ulanguzi wa ngono na ulaghai. Kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha Manhattan baada ya kunyimwa dhamana.


Katika taarifa yake, Janice Small Combs alimtetea mwanaye, akisema, "Ingawa amefanya makosa siku za nyuma, kama sisi sote tulivyowahi kufanya, yeye si mnyama kama wanavyomwonesha." Aliongeza, "Inasikitisha kuona mwanangu akihukumiwa bila ukweli, bali kwa simulizi iliyotengenezwa kwa uwongo."


Taarifa hiyo inakuja siku tano baada ya kufichuliwa kwamba Sean Combs anaweza kukabiliwa na mashtaka kutoka kwa zaidi ya watu 100, wakiwemo wanaume na wanawake, kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji. Wakili wa mwanamuziki huyo amekanusha mashtaka hayo, akiyataja kuwa ni ya "uongo na kashfa."


Sean Combs amekuwa akikabiliwa na kesi kadhaa tangu mwaka jana, ambapo mpenzi wake wa zamani, Cassie Ventura, alimshitaki kwa madai ya ubakaji na unyanyasaji wa kimapenzi. Combs alikanusha vikali tuhuma hizo, na kesi hiyo ilimalizika nje ya mahakama siku moja baada ya kuwasilishwa.

No comments:

Post a Comment