Wednesday, October 2, 2024

Iran Yashambulia Israel kwa Makombora Kufuatia Mauaji ya Viongozi wa Hamas na Hezbollah

Baadhi ya makombora yaliyorushwa na Iran yakiwa angani juu ya Israel, muda mfupi kabla ya kugonga ardhi Jumanne jioni, Oktoba 1, 2024.


Katika hatua inayozidisha mzozo wa Mashariki ya Kati, Iran imefanya shambulizi kubwa la makombora dhidi ya Israel, ikilenga "malengo ya kiusalama na kijasusi" ndani ya taifa hilo. 


Jeshi la Israel limethibitisha shambulizi hilo, likieleza kuwa lilianza saa moja na nusu jioni kwa saa za huko, likidumu kwa takriban nusu saa. Takriban makombora 180 yalirushwa na Iran.


Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, chombo cha habari cha serikali ya Iran, IRNA, kilionyesha video za mashambulizi hayo kupitia ukurasa wake wa Telegram. 


Shambulizi hilo linahusishwa na hatua ya kulipiza kisasi kutokana na mauaji ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, mjini Tehran mwezi Julai, pamoja na mauaji ya makamanda wa Hezbollah nchini Lebanon.


Taarifa kutoka Iran zimedai kuwa shambulizi hilo liliidhinishwa na Baraza la Usalama la Kitaifa la Iran, ambalo liko chini ya ofisi ya kiongozi mkuu wa taifa hilo, Ayatollah Ali Khamenei. 


Aidha, hatua hiyo pia ni jibu kwa kifo cha kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa wiki iliyopita na Israel kusini mwa Beirut.


Iran inasema kuwa shambulizi hilo ni ishara ya hasira kutokana na kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya viongozi wa muungano wa makundi ya Waislamu yanayopinga uwepo wa Israel, huku makamanda wake wa kijeshi wakishambuliwa na kuuawa na vikosi vya Israel. 


Brigedia Jenerali wa Iran, Abbas Nilforoushan, pia aliuwawa wakati wa mashambulizi hayo.


Israel bado haijatoa tamko rasmi kuhusu mauaji ya Haniyeh wala Nasrallah, lakini inajulikana kuwa taifa hilo mara nyingi hufanya mashambulizi ya kulenga wapinzani wake katika kanda ya Mashariki ya Kati.


Mzozo kati ya Israel na Iran ni sehemu ya mgogoro mpana unaohusisha mataifa ya Kiislamu ya kieneo na uhasama wa muda mrefu kati ya Israel na mataifa yanayounga mkono makundi ya wapiganaji ya Hamas na Hezbollah. 


Tangu kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948, kumekuwa na uhasama mkubwa kati yake na majirani zake wa Kiarabu, huku Iran ikionekana kama moja ya wapinzani wakubwa wa Israel.


Iran imekuwa ikiunga mkono makundi ya wapiganaji kama vile Hamas huko Palestina na Hezbollah huko Lebanon, ambayo yamekuwa yakipambana na Israel kwa muda mrefu. 


Aidha, Israel mara nyingi imehusishwa na mashambulizi ya siri yanayolenga kudhoofisha ushawishi wa Iran katika kanda hiyo, hususan kupitia mauaji ya makamanda wa kijeshi na wanasiasa wanaounga mkono uasi dhidi ya Israel.


Katika miaka ya hivi karibuni, mashambulizi ya kulipiza kisasi yamezidi kuongezeka, huku Iran na Israel zikionekana kuingia katika mzozo wa wazi zaidi wa kijeshi. Shambulizi la Jumanne ni mwendelezo wa hali ya taharuki kati ya mataifa haya mawili, hali inayoongeza hofu ya mzozo huo kusambaa zaidi kieneo.

No comments:

Post a Comment