Friday, August 2, 2024

Mauaji ya Haniyeh na Bomu lililotegwa Miezi Miwili : Ripoti ya The New York Times

 



Katika mkusanyiko wa magazeti leo, The New York Times imechapisha ripoti inayozungumzia mauaji ya kiongozi wa Palestina, Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas. 


Ripoti hiyo inadai kuwa mauaji yalitekelezwa kwa kutumia kilipuzi ambacho kilisafirishwa kwa siri hadi kwenye nyumba ya wageni ya Walinzi wa Mapinduzi ya Iran mjini Tehran miezi miwili iliyopita.


Ripoti hiyo inategemea taarifa kutoka kwa maafisa saba wa Mashariki ya Kati, wakiwemo Wairani wawili pamoja na afisa wa Marekani. 


Watano kati ya maafisa hao walithibitisha kuwa bomu hilo lililipuliwa kwa mbali, baada ya kuthibitisha kuwa Haniyeh alikuwa chumbani mwake.


Kwa mujibu wa maafisa wa Mashariki ya Kati, Haniyeh alikuwa akikaa katika nyumba hiyo ya wageni mara kadhaa wakati wa ziara zake mjini Tehran. 


Ingawa Israel haijakiri kuhusika na mauaji hayo, mashirika yake ya kijasusi yaliifahamisha Marekani na serikali nyingine za Magharibi juu ya undani wa operesheni hiyo.


Uvumi uliokuwepo ulidai uwezekano kwamba Israel ilimuua Haniyeh kwa shambulio la kombora kutoka kwa ndege isiyo na rubani, sawa na kombora lililorushwa kwenye kambi ya kijeshi huko Isfahan mwezi Aprili. 


Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa safari hii operesheni hiyo ilitumia mwanya tofauti wa usalama katika jengo la makazi ambalo lilipaswa kulindwa vikali, lakini liliruhusu bomu kufichwa kwa miezi miwili kabla ya kulipuliwa.


Ripoti hiyo haijatoa maelezo kamili kuhusu jinsi bomu hilo lilivyofichwa katika nyumba hiyo ya wageni, lakini inaeleza kuwa mauaji hayo yalichukua miezi kadhaa kupangwa na kuhitaji ufuatiliaji wa kina wa boma hilo.


Maafisa wawili wa Iran walionukuliwa na gazeti hilo walisema kuwa hawakujua jinsi au lini vilipuzi hivyo vilitegwa kwenye chumba hicho. Mlipuko huo ulitokea saa 2 asubuhi kwa saa za huko, na wafanyakazi wa jengo hilo walikimbilia kutafuta chanzo cha kelele hiyo kubwa, hadi walipofika kwenye chumba cha Haniyeh.


Timu ya madaktari katika jengo hilo ilikimbilia chumbani mara baada ya mlipuko, na kutangaza kwamba Haniyeh alikufa mara moja. Walijaribu pia kumfufua mlinzi wake, lakini pia alikufa.


Kiongozi wa harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina, Ziad al-Nakhalah, alikuwa anakaa karibu, lakini chumba chake hakikuharibiwa sana, ikionyesha mipango makini katika kumlenga Haniyeh haswa, kwa mujibu wa makala hiyo.


Ripoti hiyo inamalizia kwa kueleza kuwa usahihi na ustadi wa shambulio hilo ni sawa na mbinu ya silaha ya roboti yenye udhibiti wa mbali ambayo Israel ilitumia kumuua mwanasayansi mkuu wa nyuklia wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh, mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment