Tajiri mkubwa barani Afrika, Aliko Dangote, amewashangaza watu wengi nchini Nigeria kwa kusema hana nyumba nje ya nchi hiyo. Bw. Dangote alisema ana nyumba mbili tu, moja katika mji aliozaliwa wa Kano na nyingine Lagos, na hukodisha nyumba kila anapotembelea mji mkuu, Abuja.
Dangote aliorodheshwa na jarida la Forbes mwezi Januari kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya matatizo ya kiuchumi nchini Nigeria. Utajiri wake uliongezeka kwa $400 milioni mwaka jana, na kumpa thamani ya jumla ya $13.9 bilioni (£10.7 bilioni), kulingana na Forbes.
Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 66 alijitajirisha kupitia biashara ya saruji na sukari, na mwaka jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta katika kitovu cha uchumi cha Nigeria, Lagos. Alibainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote Jumapili.
Maoni yake yaliwashangaza wengi katika nchi ambayo watu matajiri wanajulikana kwa maisha ya kifahari, huku wengi wao wakimiliki nyumba London, Dubai, na Atlanta. Matamshi ya Dangote yamezua hisia nyingi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wengine walisema ni uamuzi wa busara wa kibiashara kwani ni nafuu kulipa kodi kuliko kununua nyumba.
Bw. Dangote alisema sababu ya uamuzi wake ni kwamba anataka kuona Nigeria ikikua. "Sababu ya kutokuwa na nyumba London au Marekani ni kuwa nilitaka kuangazia ukuaji wa viwanda nchini Nigeria," alisema. "Nina shauku kubwa juu ya ndoto ya Nigeria na kando na nyumba yangu ya Lagos, nina nyumba nyingine katika jimbo langu la Kano, na nyingine ya kukodi huko Abuja. Ikiwa nitakuwa na nyumba kote Marekani na kwingineko, singeweza kutuliza akili na kufanya kitu kwa ajili ya watu wangu."
Mchanganuzi wa masuala ya umma, Sani Bala, alisema Bw. Dangote alikuwa akionyesha mfano mzuri sana. "Wanigeria wanahitaji kuelekezwa upya kuelewa kwamba kumiliki majumba kadhaa sio mafanikio wakati pesa zingehitajika mahali pengine. Dangote alisema aliuza nyumba yake huko London mnamo mwaka 1996 na nina uhakika pesa zilizopatikana kutokana na mauzo zilirejeshwa katika biashara yake – huo ndio mfano wa kuiga."
Bw. Dangote anajulikana kumiliki makazi ya kifahari katika Kisiwa cha Banana maarufu cha Lagos, ambako Wanigeria wengi wenye hadhi ya juu pia wana majumba ya kifahari.
0 Comments:
Post a Comment