Naibu Waziri Mbarouk Nassor Mbarouk Ajiuzulu Ubunge




 


MBUNGE wa kuteuliwa na Rais na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, amejiuzulu ubunge.


Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge, ilieleza kwamba Balozi Mbarouk amemuandikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, barua ya kujiuzulu ubunge tarehe 21 Julai, 2024.


Kwa mujibu wa barua aliyomuandikia Spika, Balozi Mbarouk alisema amefikia uamuzi huo kufuatia changamoto za kijamii zinazomkabili kwa sasa.


"Ninalazimika kuchukua uamuzi wa kujiuzulu ili nipate nafasi ya kushughulikia changamoto hizo," alisema Balozi Mbarouk katika barua yake ya kujiuzulu ubunge.


Kwa uamuzi huo, Mbarouk anapoteza sifa ya kuwa Naibu Waziri, huku uamuzi huo ukimpa Rais Samia Suluhu Hassan nafasi ya kuteua MBUNGE mwingine wa kuteuliwa na Rais.


Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Rais ana nafasi ya kuteua wabunge 10.

0 Comments:

Post a Comment