Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza uamuzi wa kusitisha kampeni yake ya kuwania muhula wa pili wa urais, akisema amefanya hivyo kwa "maslahi ya chama chake na nchi."
Uamuzi huu umekuja baada ya miezi kadhaa ya mjadala ndani ya chama cha Democrats kuhusu uwezekano wa Biden kugombea tena, hasa baada ya mjadala wake na Donald Trump mwishoni mwa Juni ambao ulizua maswali mengi kuhusu uwezo wake wa kuendelea na kampeni.
Katika barua aliyoituma kupitia mitandao yake ya kijamii, Biden ameeleza heshima yake kwa jukumu la kuwa rais na jinsi alivyofurahia kutumikia nchi yake.
Amesema, "Japo ilikuwa ni azma yangu kuwania muhula wa pili, naamini itakuwa ni manufaa kwa chama changu na nchi mimi kujiengua na kujielekeza katika kukamilisha majukumu ya Urais kwa kipindi kilichosalia cha muhula wangu."
Biden amemshukuru Makamu wake Kamala Harris kwa ushirikiano wake, akimtaja kuwa "mshirika wa kipekee." Aliahidi kulihutubia taifa kuhusu uamuzi wake huo juma lijalo.
Rais huyo alirejea nyumbani kwake huko Delaware wiki iliyopita baada ya kuambukizwa virusi vya Covid-19. Aliporejea, alieleza matarajio yake ya kurejea kwenye kampeni, lakini uamuzi wake wa kujitoa umetokana na tafakari ya kina juu ya maslahi ya kitaifa na mustakabali wa chama chake.
Kwa upande wake, Donald Trump, mgombea wa chama cha Republican, amejibu uamuzi wa Biden kupitia jukwaa lake la Truth Social, akisema Biden "hakuwa sawa kugombea urais."
Hii inakuja wakati wa kushangaza katika siasa za Marekani, huku uchaguzi mkuu ukikaribia na chama cha Democrats sasa kinakabiliwa na changamoto ya kumtafuta mgombea mpya wa urais.
Joe Biden alikuwa ameelezea awali kwamba ni "Mwenyezi Mungu" pekee ndiye anayeweza kumfanya ajiondoe kwenye kampeni, lakini baadaye alisema angefikiria kujiondoa ikiwa atakuwa na sababu za kiafya.
Uamuzi wake umewashangaza wengi lakini pia umepokelewa na heshima kubwa kutoka kwa wafuasi wake na viongozi wenzake wa chama cha Democrats.
0 Comments:
Post a Comment