UPEPO MKAVU WA PWANI UNAVYOATHIRI THELUJI MLIMA KILIMANJARO


UHARIBIFU wa mazingira kwenye mikoa ya pwani unachangia kwa kiasi kikubwa kuleta madhara kwenye mlima Kilimanjaro ikiwemo kusababisha barafu kwenye mlima huo kuyeyuka.



Hayo yameelezwa leo Februari 21,2023 na Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, amishna Msaidizi wa Uhifadhi, Angela Nyaki,wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Hifadhi za Taifa nchini,(TANAPA) jijini Arusha juu ya maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa hifadhi hiyo.

Amesema kuwa hiyo imebainika baada ya tafiti zilizofanywa na kuonyesha kuwa wananchi wa maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi wanavyokata miti ardhi inabaki wazi hivyo upepo unaoelekea mlima Kilimanjaro unakuwa mkavu na wenye joto hivyo kuyeyusha barafu hiyo.


"Tafiti zinaonyesha mlima unaathirika na ukame unaotoka mikoa ya pwani. Wanakata sana miti kutengeneza mikaa, wanavyoacha ardhi inakuwa wazi upepo wa kule unavyokuja huku Kilimanjaro ukiwa mkavu na joto unafanya  barafu inaendelea kupungua," amesema Nyaki. 

Amesema kuwa  ni jukumu la nchi nzima kuhakikisha inatunza mazingira kwa sababu mikoa ya pwani haiko karibu na mlima Kilimanjaro ila wanapoharibu mazingira mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika unaathirika.


"Tumefuatilia, tukaona kukiwa na upepo mkali sana baharini na mlimani (kilele cha mlima Kilimanjaro) kunakuwa na upepo mkali. Kukiwa na mvua baharini na mlimani kunakuwa na mvua hivyo utaona kabisa kuna uhusiano wa za baharini na za mlimani," amesema Nyaki na kuongeza .

....Tukihifadhi mazingira kuanzia kwenye mikoko, misitu yote ambayo inaambaambaa na mwambao wa bahari ya Hindi itasaidia kuleta upepo wa unyevu siyo mkavu,".

KINAPA ina ukubwa wa kilometa za mraba 1,712 ikiwa  umbali wa kilometa 45 kutoka Moshi Mjini ambapo hifadhi hiyo imezungukwa na ukanda wa msitu ulio mita 1,820 kutoka usawa wa bahari.

Mlima huo unajumuisha vilele vitatu Shira, Mawenzi na Kibo ambapo kilele cha Kibo chenye urefu wa mita 5,895 ndiyo kivutio kikubwa cha watalii  wanaopanda mlima huo kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na kufunikwa kwa theluji kipindi chote cha mwaka.

Aidha kilele cha Shira kilichopo upande wa magharibi kina urefu wa mita 3962, huku kilele cha Mawenzi kilichopo upande wa mashariki kina urefu wa mita 5149.

Mlima Kilimanjaro ni moja kati ya milima ambayo kilele chake hufunikwa na theluji mwaka mzima hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wapanda milima kutoka pande zote za dunia ambapo wastani wa watalii 50,000 hupanda mlima huo kwa mwaka. 


0 Comments:

Post a Comment