Sunday, May 29, 2022

TELEZA ALIVYODAKWA NA KUUAWA ARUSHA


MTU mmoja anayedaiwa kuwa teleza ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kukurupushwa akijaribu kumwingilia binti  mmoja mkazi wa Sojema, Kata ya Murieti Jijini Arusha.


Tukio hilo limetokea Mei 29, 2022 majira ya kati ya saa nane na 10 alfajiri, ambapo ameuawa na wananchi baada ya kukamatwa katika nyumba ya moja ya wakazi wa eneo hilo akijaribu kufanya uhalifu.

Wakazi wengi wanamhusisha na mtu huyo na ajulikanae kama 'Teleza' anayetuhumiwa kuwaingilia wanawake kinguvu hasa nyakati za usiku kutokana na kukutwa amebeba mafuta anayotumia kuwaingilia kimwili wanawake huku akiwa hana shati.



Mtu huyo mrefu mweupe ambaye jina lake halikujulikana amekurupushwa na baadhi ya wakazi wa Murieti kwa kushirikiana na vijana wa sungusungu ambao kwa muda wamekuwa wakifanya doria kumsaka teleza anayedaiwa kuwa kwenye eneo hilo.



Balozi wa mtaa wa Hekaheka, Josephine Hanjewele amesema kuwa teleza huyo alikuwa anawafanya waishi kwa hofu .

Amesema mara baada ya kukamatwa kwa teleza huyo majira kati ya saa nane na tisa usiku  alipohojiwa alidai kuwa alikuwa anatoka disko Masai pub.

"Alikurupushwa mtaa wa pili alipokuja huku kwetu sungusungu wakamdaka," amesema Henjewele akizungumzia namna teleza huyo alivyonaswa.

 Mwananchi mwengine wa eneo hilo, Joan Mapunda alidai kuwa walikuwa wakiishi kwa hofu kwani teleza huyo alikuwa akiingia kwenye nyumba zao akiwakuta wamevaa nguo anawavua na kuwangilia kwa nguvu.

Inadaiwa Teleza huyo mara baada ya kukamatwa alipekuliwa alikutwa na mafuta anayoyatumiaga kwenye kuwaingilia wanawake.

Katika kujiridhisha kuwa kijana huyo aliyekuwa mweupe mrefu kuwa ndiye anahusika na matukio hayo waliitwa wahanga wa matukio hayo akiwemo binti aliyejaribu kumwingilia ingawa hakufanikiwa pamoja na mwingine aliyemwingilia siku ya sikukuu ya Pasaka  wote wakathibitisha ni mtu huyo waliyemuona.

Mwanamke aliyeingiliwa siku ya sikukuu ya Pasaka alidai kuwa siku hiyo walipambana hali  iliyosababisha teleza akatwe na dirisha ambapo walipompekua kweli alama hiyo ilionekana kwenye mwili wake.



Mkazi wa mtaa wa Muriet, Husna Mchonga anasema kuwa hii ni mara ya pili teleza huyo anakamtwa kwani mara ya kwanza alipokamatwa alipelekwa polisi lakini akaachiwa kwa kile walichoelezwa kuwa kulikosekana ushahidi wa kumshitaki.

Anasema kuwa ajira ya saa nane usiku jirani yake aliingiliwa na teleza ambaye aliingia chumba cha watoto akawataka wasipige kelele huku akiwatisha kuwa atakayekaidi atamchoma na bisibisi.

Mchonga anasema hata hivyo mtoto huyo alipiga kelele hali iliyomlazimu teleza huyo kukimbia akiwa kavaa kaptula ya bluu bila shati ndipo akakamatwa na sungusungu wa mtaa wa Hekaheka.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Murieti, Dominic Kivuyo ametoa onyo kwa wahalifu kutifika kwenye mtaa huo akisisitiza "kibaka atakayeingia mtaa wa Murieti ama zetu ama zake,".

Amesema kuwa teleza huyo alikamatwa baada ya wananchi kumkurupusha ambapo sungusungu walimsimamisha akakataa kusimama akaendelea kukimbia akiwa hana nguo ambapo alipanda ukuta kwenye nyumba tatu tofauti kabla ya kukamatwa

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi  kwani wanaweza kuua asiyehusika.

Amesema ni vema wakaacha upelelezi ufanyike kuthibitidha kama kweli wanayemtuhumu amehusika na tukio badala ya kumuua kama walivyofanya kwani inawezekana mtu akahisiwa akapigiwa kelele kwa jambo ambalo hakuhusika.



No comments:

Post a Comment