ALIYEKUWA Mgombea Urais, wa Chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe, kwenye uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 amerejea rasmi kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amerejea leo May 29, 2022 kabidhiwa kadi ya chama hicho na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, , Shaka Hamdu Shaka katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Mtama, Nape Nape Nnauye uliofanyika katika kata ya Chipomda mkoani Lindi.
Shaka alisema Membe amerejeshwa CCM baada ya kufuatwa kwa utaratibu ikiwemo kujadiliwa na tawi lake kisha na vikao vya juu.
Alisema kurejea kwa Membe ndani ya CCM kuendelee kuwa chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususan kwa wana CCM wa Jimbo la Mtama.
Kwa upande wake Membe ameeleza jinsi alivyoumia kutokana na uamuzi wa kumuondolea uwanachama wa CCM na kuahidi kufia ndani ya chama hicho ambacho ndicho kilichomlea.
Alisema Machi 30 hadi Aprili 1, mwaka huu aliitwa Dodoma, kwenye Mkutano wa Kamati Kuu ya Maadili na Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu, alipewa nafasi na Mwenyekiti wa CCM Taifa kuzungumza na wana CCM.
“Mama yetu, Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa alinipa nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa kamati kuu ya Chama Taifa. Nashukuru kwa kupewa nafasi ile na wajumbe waliliridhia kwa kauli moja nirejee CCM," amesema Membe na kuongeza.
... Nimerejea CCM kwa sababu kuu mbili, sababu ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini zote, nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa, nilishauriwa na marafiki zangu wote nirejee CCM, nilishauriwa na wana CCM,".
“Kutokana na ushauri wote huo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kutii, nimekubaliana na ushauri wa wote waliosema nirudi CCM na sasa nimerudi CCM,” .
Membe amesema sababu nyingine ya kurudi CCM inatokana na dhamira yake ya kukitumikia chama hicho tawala hadi atakapokwenda kaburini.
“Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana, nilisonekana sana, na ninyi wananchi msikitika, mlisononekana. Sababu ambazo zilinifanya niondoke CCM haziko tena, narudi sababu zilizoniondoa CCM haziko tena,".
"Nimerudi, namshukuru Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Kamati Kuu kunirudisha. Nimerudi kwenye Chama ambacho nimezaliwa na kukulia, chama ambacho kimenisomesha," amesema Membe na kuongeza.
... Hivyo niahidi sitaondoka tena, nitabakia CCM hadi mwisho wa uhai wangu. Kurudi kwangu CCM nitaendelea kukitumikia Chama changu na sasa nitaendelea kushirikiana na Mbunge wangu Nape Nnauye,".
"Mwaka 2015 nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo sasa Mtama mtakuwa na wabunge wawili, Mbunge wetu Nape na mimi mbunge wa chini chini.”

No comments:
Post a Comment