MAJALIWA AKOSHWA NA UJENZI UFUNDI TOWER YA ATC

 




WAZIRI Mkuu,  Kassim Majaliwa amelezea kuridhishwa na viwango vya ujenzi wa jengo la mnara wa ufundi (Tower) katika chuo Cha ufundi Arusha (ATC) pamoja na namna chuo hicho kinavyotumika kutoa ushauri wa kitaalam kwenye ujenzi wa majengo mengi ya serikali yanayojengwa  maeneo mbalimbali nchini.


Aidha amesema kuwa  serikali inaendelea kufanyia mapitio utaratibu  wa mikopo ya elimu ya juu ili kuona ni kwa namna gani wanafunzi wa vyuo vya kati wataweza kunufaika nayo.



Majaliwa ameyasema hayo juzi jijini Arusha wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la mnara wa ufundi (Tower) unaojengwa kwa fedha toka serikali kuu na nyingine ni fedha zao za ndani.


Amesema kuwa kwa sasa mikopo inatolewa kwa wanavyo wa vyuo vikuu lakini inawaacha wale wa vyuo vya kati ambao ni muhimu sana huku akitolea mfano kwenye ujenzi wa majengo wale walihitimu vyuo vikuu hutoa maelekezi wakati wale waliohitimu vyo vya kati ndiyo hufanya kazi nzima ya ujenzi.


Majaliwa amesema kuwa  ameridhika na ujenzi wa jengo hilo linalojumuisha maabara, madarasa, pamoja na  kliniki  itayowahudumia watumishi, wanafunzi, watumishi wa taasisi hiyo pamoja na wananchi wa Arusha walio karibu na chuo hicho na kuahidi kuwa wataendelea kuleta fedha za ujenzi katika chuo hicho ili kupunguza changamoto ya mabweni.


Waziri Miuu amesema kuwa serikali imetoa fedha za kutosha kwenye sekta ya elimu  kuanzia chekechea kwa wanafunzi wa kawaida na wenye mahitaji maalum ambapo kwa sekondari wameanza kwa kujenga madarasa na sasa wanajenga mabweni ili kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi wa kike na wakiume.



Kwa upande wake Kaimu mkuu wa chuo cha ufundi Arusha, Dkt Musa Chacha amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo ulianza Julai 2021 baada ya kupokea shilingi bilioni 1.449 kama ruzuku ya fedha za maendeleo kutoka serikali kuu.


Amesema kuwa fedha zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 428 ambapo lengo la mradi huo ni kuongeza fursa na idadi kwa wanafunzi wa kike. 


Amesema chuo kilitenga bilioni 1.036 ya mapato yake ya ndani mwaka wa fedha 2021/2022 ili kujenga kliniki ya tiba inayolenga kuboresha utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi wanaosoma programu ya vifaa tiba ambapo jengo la ghorofa tatu na sakafu moja ya chini lenye maabara, madarasa, ofisi na stoo ambalo limepewa jina la Ufundi Tower.


0 Comments:

Post a Comment