MAJALIWA AISHUKIA MSD 'UPIGAJI' FEDHA ZA UVIKO 19


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuna matumizi mabaya fedha za UVIKO 19 zilizopelekwa kwenye Bohari ya Dawa ya Taifa, (MSD)  hivyo ameiagiza Bodi ya Wataalamu ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kuwachukulia hatua haraka waliohusika.

 

 

Aidha ameahidi kutembelea MSD Jumatatu Mei 9 mwaka huu akiambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupata maelezo ya kina juu ya wizi huo.

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 5, 2022) wakati akizungumza na wataalamu wa ununuzi na ugavi pamoja na wasimamizi kwenye uzinduzi wa wiki ya Ununuzi wa Umma iliyoanza leo jijini Arusha.

 

Alisema kitendo kilichofanywa na wasimamizi wa ununuzi wa umma ambao wanaaminiwa na serikali kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko hakivumiliki na kuahidi kuwa ataanza na MSD kulishughulikia suala hilo.

 

 

"Pamoja na uwepo wa taasisi zinazosimamia manunuzi yanayofanywa katika ofisi zetu, bado wasimamizi wa manunuzi hawajaona huruma kwa walioa kodi wetu kwa kuendelea kufanya manunuzi kwa gharama kubwa," alisema Waziri Mkuu.

 

Akitoa mfano alisema MSD walitakiwa kununua kipimo cha sukari, (blood glucose test) ambacho kwa bei ya kawaida ni Sh.150 ila wao wakanunua kwa Sh. 300, kipimo cha mkojo (urinalysis) bei ya kawaida Sh. 200 kimoja wao wakanunua kwa Sh. 780.

 

 

"Walitakiwa kununua kipimo kidogo cha hematolojia ya mwili, (full blood picture 3 part) kinauzwa Sh. 2,100 wao wanaonyesha wamenunua kwa bei ya zabuni Sh  4,500.

 

 

 

“Lakini pia walipaswa kununua kipimo kikubwa cha Haemolojia ya mwili bei ya kawaida ni Sh. 3,800 wao wamenunua kwa sh. 6,300,si mnaona hizi  bei zinavyokwenda watu hawana huruma na watanzania wenzao,"alisema Majaliwa

 

 

 

Aidha aliwndelea kutoa mfano wa upigaji huo kuwa  kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo ambacho kipimo muhimu sana na vingepatikana kwa wingi  kinachouzwa Sh.6,000 wao wamenunua kwa Sh 40,000.


 

Pia,alisema walitakiwa kununua seti moja ya vitendanishi kwa ajili ya awamu moja ya kusafisha damu bei ya kawaida ambayo wangepaswa kununua ni Sh. 65,000 lakini wao wamenunua kwa Sh. 189,000 

 

Majaliwa alisema MSD walitakiwa wanunue mashine ndogo ya kipimo cha haimolojia ya mwili ambacho kinauzwa Sh.milioni tano wao wamenunua kwa Sh. milioni 14.045,huku wakitakiwa kununua mshine ndogo ya kupima kemia ya mwili ambayo bei ya kawaida ni Sh.milioni 1.35 ila wao wamenunua kwa bei ya Sh. milioni 6.7.

 

 

 

“Nyingine walitakiwa kununua mashine kubwa ya kupimia kemia ya mwili ambayo bei ya kawaida ni Sh.milioni 10.5 wao wamenunua kwa Sh.milioni 49.hawa walitakiwa wanunue mashine ya kupima sukari kifaa hiki kinauzwa Sh. 7.956 wao wamenunua kwa Sh. 58,500.

  

“Hawa walitakiwa kununua mashine kubwa ya kupimia haimolojia ya mwili hiki kifaa kinauzwa Sh. milioni 20.8 lakini wamenunua Sh milioni 117,hawa pia walitakiwa wanuue kifaa kinaitwa mashine ya kupimia haimolojia ya mwili cha ukubwa kidogo bei ya kawaida ni Sh. milioni 37.4 wao wamenunua Sh.milioni 149.4.

 

 

 

"Hebu wataalamu wetu mtuambie ni kwa sababu ya nini,wataalamu wetu wa manunuzi kwa nini hili linatokea?kwa maslahi ya nani“Je tukichukua hatua tena kali,vyombo vyote mko hapa vya manunuzi haya ndiyo yanayoendelea kwenye ofisi zetu,kwa wale wachache wasio kuwa na nia njema na fedha za walipa kodi wa nchi hii,"alisema

 

 

Alisema ongezeko hilo  la fedha zilizopotea kwa ujanja wa watu wasiozingatia sheria,taratibu, kanuni za ununuzi wa umma  ambazo zingenunua vifaa kwa wingi, lakini wamenunua kifaa kimoja tu huku watanzania wanasubiri kupata vifaa vingi visambae kwenye hospitali,zahanati na vituo vya afya 

 

Aidha alisema mtu mmoja anakwamisha watanzania  kupata huduma walizotahili na ni watu walioaminiwa ba serikali kusimamia fedha za umma. 

 

 

"Jumatatu nikukute pale saa nne asubuhi wanipe maelezo  haya na mimi sitasita kwenda na Kamanda Siroo na Hamhuduni ili washughulike na ha o na tunapoanza na hao huwa hawabaki kazini,hii sio nia ya serikali yenu ila mnatulazimisha,"alisema.

 

 

 

Naibu wa Fedha na Mipango, Hamad Chande alisema serikali  imeboresha na kuondoa vifungu vilivyokuwa na vikwazo katika ununuzi wa umma.

 

 

 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa umma (PPRA) Irene  Isaka,alisema wiki hiyo ya ununuzi wa umma inakauli mbiu ya "Matumizi ya Teknolojia latika kuboresha ununuzi wa umma" na inawashiriki 1003.

 

 

Waandaaji wa mkutano huo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) na unahudhuriwa na wadau mbalimbali wa ununuzi nchini wakiwemo madiwani.


0 Comments:

Post a Comment