Sunday, May 8, 2022

KIJANA AMUUA KAKA YAKE, AMCHOMA KISU MAMA YAKE


KIJANA , Adael Willbad (21) Mkazi wa kitongoji cha Upendo  katika kijiji cha Manyire wilaya ya Arumeru ,Mkoani Arusha anadaiwa kumuua kaka yake kwa kisu  aliyekuwa akijaribu kumuokoa mama yake mzazi, Editha Vavoiyo aliyejeruhiwa tumboni  kwa kisu kwenye  ugomvi wa kugombea jiko la kupikia ambalo walishakatazwa kulitumia.




Tukio hilo linadaiwa kutokea jana  majira ya saa 1.30 jioni nyumbani kwa familia hiyo mara baada ya kuzuka mzozo baina ya marehemu ,aliyefahamika kwa majina ya Ezekiel Willbard (24) na mdogo wake (Mtuhumiwa) wakigombea jiko kwa ajili ya kupikia.


Mwenyekiti wa kijiji cha Manyire, Evarest Mallya ,alisema kuwa chanzo cha mzozo huo ulitokana na wanandugu hao kugombea sehemu ya kupikia ambapo mama yao mzazi, Editha aliwakataza na kuwaambia wakatafute sehemu nyingine ya kupikia kwa sababu jiko hilo ni mali yake.

Alisema kuwa mama yao baada ya kuona mzozo unazidi kuwa mkubwa aliamua kuchukua uamuzi wa kumwagia maji katika jiko hilo ili wote wakose jambo linalodaiwa  kumkera mtuhumiwa na kuamua kumjeruhi mama yake tumboni.


Mallya alidai kuwa  baada ya  mama huyo kujeruhiwa alianguka chini,tukio ambalo lilishuhudiwa na kaka yake (marehemu) ambaye alipoona mama yake amechomwa kisu na kudondoka chini aliingia ndani na kuchukua chuma ili kumpiga mdogo wake ,lakini wakati akitoka nje hakumwona kwa kuwa alikuwa amejificha.


"Marehemu,Ezekiel aliamua kumfuata mama yake na kujaribu kumwinua lakini wakati akielekea eneo hilo ghafla mtuhumiwa alitokea ghafla mafichoni na kumchoma kisu cha ubavuni kushoto na kuanguka chini," alisema Mallya.


Mwenyekiti alisema kuwa mtuhumiwa, Adael alimburuta na kumficha marehemu, Ezekiel kwenye shamba la mahindi kando ya nyumba yao hadi siku inayofuata ambapo  watoto wadogo waliokuwepo nyumbani waliuona mwili wa kaka yao ukiwa shambani akiwa amepoteza maisha.


Mallya alisema mtuhumiwa  huyo alijaribu kutoroka lakini wananchi walifanikiwa kumkamata katika  eneo la Gomba alikokuwa amekimbilia kujificha.


"Baada ya kufanikiwa kutoroka alienda katika kituo cha polisi Chekereni na kutoa taarifa kwamba kaka yake amemchoma kisu mama yake na sisi baada ya kupata taarifa tulianza msako wa kumtafuta na kufanikiwa kumkamata akiwa eneo la Gomba wilayani Arumeru  amejificha na tulimpeleka katika kituo cha polisi ambako hadi sasa anashikiliwa ,"alisema  mwenyekiti huyo.


Mama, Editha alimbizwa katika hospital  ya ya rufaa ya mkoa, Mt Meru ambako amelazwa akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa na kisu tumboni, na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya Nkoaranga wilayani Arumeru.



Juhudi za kumpata Kamanda wa polisi Mkoani hapa , (RPC), Justine Masejo hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita muda wote bila kupokelewa hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi akitakiwa kutoa uthibitisho wa tukio hilo hakujibu.


No comments:

Post a Comment