MWENYEKITI wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema baada ya uamuzi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki,(EACJ) kuielekeza serikali ya Tanzania kuifanyia marekebisho sheria ya Vyama vya siasa, wanaandaa kikundi cha ulinzi wa chama chao, Red Brigedi warudi kutekeleza majukumu yao.
Ameyasema hayo leo akiongea na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha yalipo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,(EAC) akiwa ameambatana na viongozi na wafuasi wa Chadema kutoka mkoani Arusha.
“ Sisi tunaendelea na harakati za demokrasia, hatukusimama hata sheria hizi mbaya zilipotungwa. Tuliendelea kufanya kazi ya siasa na tutaendelea hivyo na kudai mengine mengi zaidi wenye wajibu wa kutekeleza sheria hii siyo sisi ni serikali ya Tanzania kwa kupeleka mabadiliko bungeni ikarekebishwe ili haki ya watu iweze kupatikana kama ambavyo mahakama imefanya maamuzi hayo,” amesema Mbowe na kuongeza.
…Hatuwezi kuweka ukomo wa uvumilivu, kwa kuwa sisi hatukusimama kazi ya siasa haina maana kwamba bila mabadiliko haya kazi ya siasa haitafanyika kazi ya siasa itafanyika tu na sisi tunawaanda Red Brigedi warudi kulinda Chama chetu na haki zake kama kawaida,”.
Mbowe alishukuru jopo la majaji waiosikiliza maombi yao na kutoa uamuzi huo ambao wametoka nchi mbalimbali za EAC kwa kile alichodai kuwa uamuzi walioufikia japo wamechukua muda mrefu kidogo lakini wamefanya maamuzi ambayo anapenda kuamini kwamba yatajenga urahisi wa Watanzania kufanya demokrasia nchini kwa amani endapo itatekelezwa kama walivyoshauri .
“Mahakama hii ina uwezo wa kushauri na wameishauri mahakama ya Tanzania ifanye marekebisho hayo ya msingi ili kuruhusu kutekeleza matakwa yake kama mwanachama wa EAC,” amesema Mbowe na kuongeza.
…Naitaka serikali ya Tanzania na kipekee namtaka mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aone sheria yetu yetu ya vyama vya siasa tayari inanyooshewa macho na inanyooshewa vidole na majaji wa EAC .
… Hili ni jambo la msingi sana. Na natambua kwamba pamekuwa na malalamiko mengi ndani kwa wenyewe mabadiliko yameanza kufanyika lakini bado hayajafikia ukomo serikali ya Tanzania ijitahidi ifanyie marekenisho sheria zetu.
…Tuifanye nchi yetu ni mahali salama kwa kufanya siasa, nchi yetu ni mahali salama pa kushauriana na nchi yetu ni mahali salama kwa upana wote kwa uhuru wa watu na haki za wote ziweze kudumishwa wakati wote,”.
Kwa upande wake mmoja wa mawakili wa waleta maombi, John Mallya amesema Mahakama ya EACJ imeiamuru Tanzania ikatoe vifungu hivyo kwenye vitabu yake vya sheria ili vibaki na nafasi ya kufanya siasa kwa nafasi zaidi.
“Maombi yetu tuliyoleta mahakama ni kwamba endapo vifungu vitabaki kwenye sheria vitamkwe na mahakama kwamba havina mamlaka kisheria, vitakuwa kama urembo tu,” amesema wakili Mallya na kuongeza.
…Ushauri wetu,(serikali ya Tanzania) ifanye hivyo ilivyoagizwa na mahakama kwa sababu ni Mjumbe wa mahakama ya EACJ na mahakama hii inayo njia ya kufanya ‘enforcement’ ya kutekeleza hukumu yake.Kwa kuizuia Tanzania kushiriki kwenye vikao vya jumuiya na ku suspend uanachama wake na kuipiga faini.
…Tanzania isipotekeleza hukumu hii tutajua ni kitu gani cha kufanya (vifungu hivyo ) visiwe na nguvu kisheria kama vinabaki kwenye katiba viwe kama urembo.

0 Comments:
Post a Comment