Saturday, March 19, 2022

MAPOKEZI YA MBOWE HAYAJAPATA KUTOKEA, BARABARA YA ARUSHA MOSHI YAFUNGWA KWA MUDA

 


WANANCHI wengi mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani ya Arusha na Manyara  wamejitokeza kwa wingi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kumpokea mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA,  Freeman Mbowe.


Aidha, mapokezi hayo yalisababisha baadhi ya barabara kufungwa kwa muda kutokana na wingi wa watu, magari na pikipiki.

 

Mwenyekiti wa Chama Mhe. Freeman Mbowe  akipatiwa zawadi ya Ngao na Mkuki na wazee wa Machame.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mbowe kwenda Hai tangu atoke gerezani Machi 4, mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri la  ugaidi na uhujumu uchumi lililokuwa likimkabili Mbowe na wenzake watatu.

Siku alipotoka gerezani Mbowe, amekuwa akifanya vikao mbalimbali ambapo kikao cha kwanza ni kati yake na Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alimuita Ikulu jijini Dar es Salaam na kukubaliana kufanya siasa za kistaarabu na kujenga Taifa

Wakati wa mapokezi hayo leo shughuli mbalimbali zilisimama kwa muda wakati msafara wa Mbowe ukitoka uwanjani wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, (KIA) huku  barabara ya Arusha Moshi ikipitika kwa shida kutokana na wingi wa wtau waliojitokeza kumlaki.

 

Aidha msururu mrefu wa magari ulisababisha barabara hiyo kuwa na foleni kwa muda  ambapo Mbowe wakati anaondoka uwanja wa ndege msafara wake ulikuwa ukiongozwa na mbwa aliyekuwa ameshikiliwa na kijana mmoja.

 

Wananchi walikuwa wakitumia usafiri wa aina mbalimbali ambapo wengine walitumia  bodaboda, bajaji, magari hukuwengine wakitembea kwa miguu.

 


Wengi wa wananchi hao walikuwa wamekusanyika eneo la njia panda ya KIA huku Jeshi ka Polisi likiimarisha ulinzi na kuongoza msafara huo.


Mbowe aliyekuwa  kwenye gari la wazi ameonekana muda wote akiwa na furaha huku akiwapungia wananchi na kuwashukuru kwa kusema "asanteni kunipokea tupo pamoja" kisha msafara kuondoka kuelekea Bomang'ombe zilipo ofisi za Chadema kisha kuelekea kijijini kwake Nshara, Machame.

 

No comments:

Post a Comment