Na Arodia Peter, Dar
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeipokea kwa furaha hukumu ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (East African Court of Justice-EACJ) kuwa vifungu vya 3,4,5,15 na 29 vya Sheria ya Vyama vya Siasa, 2019 vinakiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo vinapaswa kurekebishwa.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Machi 25,2022 kwenye kesi iliyofunguliwa Mwaka 2019 na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini.
Pia chama hicho kimepongeza Mawakili wote ambao wamefanyakazi kubwa kuhakikusha ushindi huo unapatikana.
Taarifa ya chama hicho iliyosainiwa na Msemaji wa Kisekta, Katiba na Sheria, Victor Kweka leo Machi 25, 2022 imesema Sheria ya Vyama vya Siasa iliyopitishwa na Bunge mwaka 2019 inapaswa kuandikwa upya ili kuhakikisha siasa nchini zinaendeshwa kwa misingi ya haki na usawa.
"Msimamo wa ACT Wazalendo siku zote ni kuwa marekebisho ya sheria ya vyama vya Siasa yaliyofanyika mwaka 2019 hayakubaliki kwa jamii yenye misingi ya kidemokrasia kwa sababu yanajinaisha siasa na kuipa madaraka makubwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa.
...Sisi ACT Wazalendo tunarejea wito wetu wa siku zote kuwa Sheria ya Vyama vya siasa iandikwe upya ili siasa nchini ziendeshwe kwa misingi ya Usawa" amesema Kweka.
Viongozi waliofungua kesi kwa niaba ya vyama 10 vya upinzani nchini ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad (R.I.P), Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHAUMMA, Hashim Rungwe pamoja nai Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Salum Mwalim.

No comments:
Post a Comment