Serikali imetoa miezi mitatu kwa wenye shehena ya vifungashio visivyokidhi viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) vinaondolewa sokoni.
Agizo hilo limetolewa Januari 8, 2020 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Ofisi hiyo jijini Dodoma kuhusu matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kama vibebeo vya bidhaa.
Ummy alisema hatua hiyo ya Serikali imechukuliwa baada ya kuwepo kwa vifungashio vinavyotumika kama vibebeo vilivyozagaa madukani, sokoni na maeneo mbalimbali.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na katazo la mifuko ya plastiki siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya tubings visivyokuwa na sifa na hivyo kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na TBS.
Aidha, Waziri Ummy aliongeza kuwa vifungashio hivi kwa sasa vinazalishwa kwa wingi na kwa ukubwa mbalimbali na vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni na kuleta dhana kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine kama “vifungashio”.
Alisema mifuko hii imeanza kuzagaa kwenye mazingira ya mitaa yetu na vijiji vyetu kwa kasi kubwa, na hivyo kurudisha nyuma mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi chote cha kupambana na changamoto ya mifuko ya plastiki.
Kwa mantiki hiyo Waziri Ummy aliwataka wasambazaji, wazalishaji wa vifungashio hivi na waagizaji kuacha mara moja kuzalisha, kusambaza, kuuza na kutumia vifungashio hivyo na kusisitiza kuwa baada ya kipindi hicho Serikali haitatoa tangazo lingine lolote kuhusiana na katazo la matumizi ya vifungashio visivyokuwa na ubora.
Waziri huyo alisema Serikali itachukua hatua kali kwa mujibu kisheria na katika kipindi hiki tunaendelea na operesheni maalumu kuwabaini wanaokwamisha mafanikio haya kwa kuzalisha na kusambaza vifungashio hivyo na hatutawavumilia watu hawa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo alisema Ofisi hiyo itashirikiana na TBS kuanza kampeni ya kupitia tena mifuko ya ‘non woven’ kwani kuna uwezekano wa kuwepo kwa mifuko isiyo na viwango.
Malongo alisema Serikali ilipoweka katazo la mifuko ya plastiki iliweka pia viwango vya mifuko ya aina hiyo akitaja kuwa ni lazima iwe na uzito wa gramu 70 kwa mita ya mraba moja ili itumike kwa zaidi ya mara moja.
Aliongeza kuwa pia lazima mifuko hiyo iwe na nembo ya TBS ili kuonesha kuwa imekidhi vigezo vinavyotakiwa pamoja na kutambulisha jina la mzalishaji.
Kigezo Kingine ni viwe na lakiri (Seal), ikimaanishwa kuwa kifungashio kinatakiwa kifungashwe na anayefungasha bidhaa yake ili kuuza kabla ya kwenda sokoni.


No comments:
Post a Comment