Sunday, December 27, 2020

MAJALIWA ASIMAMISHA WAWILI PTA , AMUAGIZA CAG AFANYE UKAGUZI MAALUM

 


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Tanga na Kyela kutokana na kuwepo madai ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

 

Aidha  amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa TPA,  Nuru Mhando pamoja na Meneja wa Matumizi ya Fedha wa TPA,  Witness Mahela ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazowakabili.


Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada kupokea ripoti ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na CAG katika hesabu ya Bandari ya Kigoma kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019. Lengo la ukaguzi huo lilikuwa kujiridhisha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.

 

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Desemba 27, 2020) katika kikao chake na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kilichofanyika katika ofisi za TPA jijini Dar es Salaam. 

Amesema taasisi hiyo imebeba taswira ya uchumi wa Taifa, lazima kazi ifanyike vizuri.

 

 Majaliwa ameitaka Bodi ya PTA  ihakikishe mamlaka hiyo inafanya kazi kwa weledi na isisite kuchukua hatua kwa mtumishi atakayebainika kutenda makosa na isimbebe kwa namna yoyote.

No comments:

Post a Comment