WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Dk.Harrison Mwakyembe amewataka maafisa habari serikalini kuhakikisha wanatimiza ipasavyo majukumu yao ya kuhabarisha umma juu ya mambo yanatekelezwa na serikali vinginevyo hatasita kupeleka majina yao kwa waziri mkuu ili watumbuliwe.

Aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akifungua mkutano wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini, (TAGCO) unaofanyika kwa siku tano jijini Arusha chini ya mwenyekiti wao, Paschal Shelutete.


Dk Mwakyembe aliwataka Maafisa Mawasiliano hao kuhakikisha wanajituma kwa kutoa taarifa za kazi zinazofanyika kila siku na taasisi zao  kwenye mitandao ya kijamii na endapo watazuiwa na mtu yoyote wasisite kuwafichua hata kwa siri ili Wizara yake iweze kuwashughilikia hao watakaobainika kuhusika.


"Kweli naangalia Tovuti za halmashauri zipo tisa tu zinazofanya vizuri nyingine  wahusika  wamelala na Mikoa 18 tu ndiyo inafanya vizuri kuhabarisha, sasa hawa wengine wajitathimini vinginevyo nitapeleka majina yao kwa Waziri Mkuu ili watumbuliwe tutoe ajira kwa wengine,"alisema Dk Mwakyembe.

Alisema  maafisa habari wasiotimiza wajibu wao hawana tofauti  na watumishi hewa ambao wanakula mishahara wasioifanyia kazi,jambo ambalo aliweka bayana kuwa hakubaliani nalo huku akiwaonya wasigeuze  tovuti walizonazo kuwa magofu bali ziwe majokofu ya kuhifadhia habari



Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAGCO Pascal Shelutete alisema lengo la kikao hicho cha kazi ni kukuza mawasiliano baina ya maafisa hao wa serikali na kukuza ufahamu wa wananchi juu ya  kazi za serikali.

Aidha alisema wamefikia makubaliano Umoja wa Mataifa nchini, (UN Tanzania) ya kushirikiana katika nyanja za masiliano kwa lengo kuimarisha na kuboresha utendaji kazi ambapo makubaliano hayo yanatarajiwa kusainiwa leo.


Akiongea kwenye mkutano huo Mwakilishi  Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez, kutokana na kukua kwa kasi kwa teknolojia yamawasiliano jamho alilodai kuwa ambapo pia kumepelekea wakati mwingine kuwepo kwa taarifa za uongo.

"Hivyo basi serikali ina umuhimu mkubwa wa kufundisha, kuhabarisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia inayotuunganisha. Lakini Serikali hiyo hiyo, inahitaji kusikiliza jamii, kwani ni sauti za wananchi na hii itafanikisha kupata maendeleo ya haraka Tanzania," alisema Rodriguez.

Alisema wanapenda kushirikiana na Serikali katika mawasiliano ya maendeleo hapa nchini kwani moja ya majukumu yao ni kusaidia katika kutekeleza malengo ya dunia ambapo leo wataingia makubaliano rasmi ya TAGCO ikiwa ni kuhakikisha wanaonyesha matokeo chanya yanayofanywa na Serikali.

0 Comments:

Post a Comment