Wizara ya Ulinzi ya Japani imesema kombora lililorushwa na Korea Kaskazini Ijumaa usiku huenda lilikuwa aina ile ile ya kombora linalovuka mabara, ICBM, lililorushwa na nchi hiyo Julai 4 mwaka huu.
Wizara hiyo inaamini kombora hilo lililorushwa kutoka kijiji cha Mupyong-ri takribani saa tano na dakika 42 usiku, lilisafiri umbali wa takribani kilomita 1,000 kaskazini mashariki na kuangukia kwenye ukanda maalum wa kiuchumi wa Japani takribani kilomita 150 kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Okushiri kwenye Bahari ya Japani.
Inakadiria kuwa kombora hilo lilisafiri kwa dakika 45 na kufikia umbali wa kilomita zaidi ya 3,500 kutoka usawa wa bahari, ukiwa ni umbali mrefu zaidi kuwahi kufikiwa na makombora yaliyorushwa na Korea Kaskazini.
Wizara ya Ulinzi ya Japani imesema kuwa kwa kuzingatia uchunguzi wa video iliyotolewa na Korea Kaskazini jana Jumamosi, kombora hilo huenda ni aina ile ile ya Hwasong-14 linaloweza kuvuka mabara, ICBM, lililorushwa na nchi hiyo Julai 4 mwaka huu.
Wizara hiyo inaamini kombora hilo huenda likawa aina ya ICBM ambalo kiwango chake cha juu cha masafa kinazidi kilomita 5,500 na urushaji wake huenda ulikuwa sehemu ya maendeleo ya makombora ya masafa marefu uliolenga kutoa onyo kwa Marekani.

No comments:
Post a Comment