Friday, May 5, 2017

TANESCO YAWAKATIA UMEME MAGEREZA , MOUNT MERU HOSPITAL I


SHIRIKA la Umeme  Nchini, (TANESCO),  mkoani Arusha, limewakatia umeme majeshi ya ulinzi na usalama mkoani hapa pamoja na hospitali zote za Serikali ikiwemo ile ya mkoa ya Mount Meru kutokana na malimbikizo makubwa ya madeni ya ankara za umeme ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4.
Taasisi ziliizokatiwa umeme jana na kiasi wanachodaiwa kwenye mabano ni pamoja na Jeshi  la Wananchi,  (TPDF) ( Shilingi milioni 538), makao
Makuu ya Polisi Mkoa na vituo vyao, ( Shilingi milioni 490) Magereza, ( shilingi milioni  271),  Jeshi la Kujenga Taifa, (JKT)- Oljoro, ( Shilingi milioni 57)  na hospitali zote za serikali, (shilingi milioni 58).
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana Afisa Uhusiano wa Tanesco Mkoani hapa, Saidy Mremi, alisema kuwa huo ni utekelezaji wa agizo la Rais   John Magufuli, kwa kuwakatia umeme wadaiwa sugu.
"Rais alituambia tuwakatie  umeme wadaiwa sugu hata kama ni taasisi za Serikali au watu binafsi bila kuogopa na alisisitiza kwa kutumia maneno haya kata hivyo Tanesco tunaendelea na operesheni hii kabambe kabisa," alisisitiza  Mremi.
Alisema kuwa operesheni hiyo inaongozwa na Meneja wa Tanesco Kanda ya Kaskazini, Mhandisi, Stella Hizza na Meneja Mkoa wa Arusha Mhandisi Gasper Msigwa .
Alisema jumla ya madeni sugu ni zaidi ya shilingi
bilioni 8.6 kwa Mkoa mzima huku majeshi yakidaiwa
asilimia 28 ya deni lote.
“Ili tuzalishe umeme wa uhakika lazima wadaiwa wetu walipe fedha tunazowadai, na sisi tuweze kuzalisha vizuri. Vinginevyo huduma haziwezi kuwa bora kama watu wanavyotaka,”alisema Mremi.
Aidha alisema kuwa  wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwa na wezi wa umeme jambo alilowaonya wale watakaopitiwa na operesheni hiyo ya kukatiwa umeme wasijiunganishie kwani wakibainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Maeneo ya Jeshi la  Polisi yaliyokatiwa umeme ni pamoja na  Makao makuu ya Polisi,
(RPC), Kituo kikuu cha Kati, Trafiki, na vituo vidogo vya polisi vya Unga limited,  Ngarenaro, Sakina, Chekereni, Ngaramtoni, Kijenge, Olorien , Mbauda na Sekei.
Aidha alisema maeneo mengine waliyokata ni maduka ya  Jeshi JKT Oljoro na lingine lililopo maeneo ya  Nanenane jijini hapa.
Jeshi la magereza nalo lilikatiwa umeme hali inayoibua maswali hali itakuwaje kwa mahabusu na wafungwa wanaohifadhiwa kwenye gereza la mkoa la Kisongo.
Rais Magufuli hivi karibuni katika muendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara aliitaka Tanesco kuwakatia umeme wadaiwa sugu huku akienda mbali kwa kusema hata kama ni IKULU inadaiwa haijalipa umeme nayo ikatiwe umeme
"Maneno ni mawili tu, KATA, iwe ni Ikulu, Jeshini, Polisi kama hawajalipia bili ya umeme wewe KATA" alisistiza Rais Magufuli
Alisema pia serikali ya Mapinduzi Zanzibar nayo inadaiwa umeme na kwa kuwa hawajalipia nao wakatiwe umeme

No comments:

Post a Comment