Wanaharakati 1,500 nchini Morocco wametangaza kufungamana kwao na Wapalestina mateka waliogoma kula ambao wanashikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa taarifa, 'Muungano wa Morocco kwa Ajili ya Wapalestina" ambao pia unapinga uhusiano wowote na utawala wa Kizayuni wa Israel umetangaza kuwa wanaharakati 1,500 wa Wamorocco katika miji 50 nchini humo wametangaza kususia kula kwa masaa 24 kama njia ya kubainisha kufungamana kwao na mateka Wapalestina waliosusia kula.
Kwa mujibu wa taarifa ya muungano huo, mgomo huo umeanza katika jengo la Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Morocco katika mji mkuu wa nchi hiyo Rabat.
Itakumbukwa kuwa, Jumla ya wafungwa 1,600 wa Kipalestina wanaoshikiliwa na utawala ghasibu wa Israel, walianzisha mgomo wa kula chakula tangu tarehe 17 Aprili, katika kulalamikia miamala mibaya na kukanyagwa haki zao za kimsingi katika jela za Israel.
Mgomo huo unaongozwa na Marwan Al-Barghuthi kwa kaulimbiu ya "Uhuru na Heshima" katika magereza yote ya utawala wa Kizayuni.
Inafaa kuashiria kuwa, zaidi ya raia elfu saba wa Palestina, wanashikiliwa katika jela za Israel huku wengine wakipitisha miaka mingi bila ya kushtakiwa wala kufunguliwa mashtaka yoyote.
Jumanne iliyopita Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah, alikosoa vikali hatua ya nchi za Kiarabu ya kufumbia macho masaibu yanayowakabili mamia ya wafungwa wa Palestina ambao kwa sasa wamesusia kula chakula kwa muda mrefu katika jela za utawala haramu wa Israel.
0 Comments:
Post a Comment