Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Wilbroad Slaa (76), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo jijini Dar es Salaam, kujibu shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa X (zamani Twitter).
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alithibitisha kukamatwa kwa Dkt. Slaa na kusema kuwa kwa sasa yupo kwenye mahojiano na polisi kuhusu baadhi ya mambo, na kwamba hatua inayofuata itategemea mifumo ya kisheria.
Kamanda Muliro alisema taarifa kamili kuhusu hali ya mtuhumiwa zitatolewa baadaye.
Taarifa za kukamatwa kwa Dkt. Slaa zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii, ikionyesha sauti ya mwanasiasa huyo akielezea tukio la kukamatwa kwake na kueleza kwamba anapelekwa katika Kituo cha Polisi cha Mbweni, Dar es Salaam.
Dkt. Slaa, ambaye aliteuliwa na Rais Hayati John Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden kuanzia Novemba 2017, alikosa wadhifa huo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumvua wadhifa huo mwaka 2023.
Pia, Dkt. Slaa alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya kujiondoa katika chama hicho mwaka 2015.
0 Comments:
Post a Comment