Wednesday, May 3, 2017

KIMATAIFA : Wajumbe waanza majadiliano kupitia mkataba wa nyuklia



Kikao cha maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa mapitio ya Mkataba wa Kuzuia Kuenea silaha za Nyuklia-NPT wa mwaka 2020 ulizinduliwa jana Jumanne kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Vienna nchini Austria. Wajumbe wa mkutano huo wana maoni tofauti kuhusiana na mkataba huo.

Zaidi ya nchi 100 zisizo na silaha za nyuklia zimekuwa kwenye majadiliano tangu mwezi Machi mwaka huu juu ya kuanzisha mkataba mpya utakaopinga kisheria maendeleo, kumiliki na kutumia silaha za nyuklia.

Hata hivyo nchi zenye nguvu ya silaha za nyuklia na washirika wake zinapinga vikali hatua hizo, zikidai hatua hiyo inapingana na ukweli kwenye jumuiya ya kimataifa.

Mwakilishi wa Austria alisema wajumbe katika mkutano wa NPT wamekuwa wakirejelea suala hilo mara kwa mara bila ya kupiga hatua. Alisema mkataba wa kupiga marufuku wa silaha za nyuklia utaimarisha NPT. Austria imekuwa ikifanya jitihada kuwezesha majadiliano ya mkataba mpya.

Mwakilishi wa Marekani alisema ni muhimu kutekeleza mkataba huo unaoweka ukomo wa umiliki wa silaha za nyuklia na kuondoa tishio la uendelezaji nyuklia la Korea Kaskazini. Mjumbe huyo alidai kuwepo mtazamo wenye uhalisia kuelekea kuachana na silaha za nyuklia ndani ya mpango kazi wa NPT. Kikao hicho cha maandalizi kitaendelea hadi Mei 12.

No comments:

Post a Comment