Friday, May 26, 2017

KIMATAIFA: Maamuzi ya Urusi kuhusu vikwazo vya Marekani kuhusu Korea Kaskazini


Kituo cha habari kinachoendeshwa na serikali ya Korea Kaskazini kimeripoti kuwa Urusi imethibitisha tena msimamo wake wa kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini.

Leo Ijumaa kituo hicho kimesema, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Han Song Ryol alikutana na Balozi wa Urusi nchini Korea Kaskazini Alexander Matsegora jana Alhamisi.

Kituo hicho kimesema kuwa Han alimwambia Balozi huyo kuwa ni jambo la dharura kusitisha mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya Marekani na Korea Kusini, na vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini ili waweze kudhibiti hali hiyo.

Aidha, kituo hicho kimesema Matsegora alielezea matumaini ya kuboresha mahusiano ya nchi mbili, akidai kuwa amedhibitisha tena msimamo wa Urusi wa kupinga vitisho vya kijeshi na vikwazo vya Marekani.

Urusi na Korea Kaskazini wamekuwa wakishirikiana kuboresha mahusiano yao katika siku za karibuni.
Pamoja na kufunguliwa kwa njia mpya ya feri kati ya nchi hizo mbili wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini ilitoa taarifa juzi Jumatano, ikiomba kuboresha ushirikiano wa kiuchumi na Urusi.

Aidha, Han na Matsegora walikutana Aprili 30 na kukubaliana kuendeleza mahusiano ya nchi hizo mbili.

No comments:

Post a Comment