HABARI: Ulikosa hii? Korea Kaskazini leo ilifanya jaribio lingine la Kombora


'Korea Kaskazini yarusha kombora lingine leo alfajiri'

Korea Kaskazini imerusha kombora mapema leo Jumapili asubuhi kutokea kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Mkuu wa Majeshi ya Korea Kusini amesema kombora hilo lilirushwa kuelekea mashariki takribani saa kumi na moja na nusu alfajiri kwa saa za nchi hiyo karibu na eneo la Kusong lililo kwenye jimbo la kaskazini magharibi la Pyongan-pukdo. 

Alisema kombora hilo lilianguka kwenye eneo la Bahari ya Japani baada ya kuruka umbali wa zaidi ya kilomita 700. Jaribio hilo lilikuwa la kwanza baada ya kuapishwa kwa rais mpya wa Korea Kusini Moon Jae-in Jumatano iliyopita. Jeshi la Korea Kusini linaendelea na zoezi la kukusanya na kufanyia uchunguzi taarifa kuhusu jaribio hilo. 

Rais Moon alimuagiza mkuu huyo wa majeshi ya Korea Kusini kuitisha mkutano wa dharura. Rais huyo wa Korea Kusini alisema kwa ajili ya amani, yuko tayari kutembelea Marekani, China, Japani na hata Korea Kaskazini kama hali itaruhusu. 

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Korea Kusini vinasema Korea Kaskazini imefanya jaribio la sasa kwa lengo la kuimarisha msimamo wake wakati huu ambapo mataifa hayo mawili yanatarajiwa kuanza majadiliano katika siku za usoni. 

Kwenye mkutano mfupi na waandishi wa habari uliofanyika leo asubuhi katibu mkuu wa baraza la mawaziri la Japani, Yoshihide Suga amesema kombora hilo linaaminika liliruka umbali wa takribani kilomita 800 kwa takribani dakika 30 kabla ya kuanguka kwenye Bahari ya Japani kilomita 400 mashariki mwa Rasi ya Korea. Alisema eneo ambapo kombora hilo limeangukia haliko ndani ya ukanda maalum wa kiuchumi wa Japani.

First viewed on NHK 

0 Comments:

Post a Comment