HABARI: Korea Kaskazini yafanimiwa kombora la Jana, Kom aionya Marekani tena


Korea Kaskazini imesema jana Jumapili ilifanikiwa kufanya jaribio la kurusha aina mpya ya kombora linalorushwa kutoka ardhini na kutua ardhini.

Gazeti la Rodong Sinmun linalomilikiwa na chama tawala cha wafanyakazi cha nchi hiyo limeonyesha kwenye makala yake ya leo Jumatatu picha za kombora hilo likiwa linarushwa kutoka kwenye eneo la kurushia makombora linalohamishika.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo limesema kombora hilo ililoliita Hwasong-12 liliruka juu umbali wa kilomita 2,111 na kusafiri umbali wa kilomita 787 na kuanguka kwenye eneo lililokusudiwa la bahari huru kwenye Bahari ya Japani. Taarifa hiyo ilisema kombora hilo lilirushwa juu zaidi kutokea pembenukta karibu na wima.

Taarifa hiyo iliendelea kusema jaribio hilo lililenga kuthibitisha maelekezo ya kiufundi ya kombora hilo la aina mpya lenye uwezo wa kubeba kichwa kikubwa cha nyuklia. 

Kombora hilo linaaminika kuwa aina mpya ya makombora ya masafa ya kati ambayo ni toleo lililotokana na utengenezaji mpya wa aina ya makombora yanayorushwa kutoka kwenye nyambizi. 

Shirika hilo la habari linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo limesema jaribio hilo lililofanyika jana Jumapili lilisimamiwa na kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Kim Jong Un.

Lilisema Kim aliionya Marekani kuwa endapo itajaribu kuichokoza nchi yake basi itashindwa kuepuka janga kubwa kuliko yote duniani. Alisisitiza kuwa Marekani bara na maeneo ya Pasifiki ambako nchi hiyo inafanya operesheni zake yote yako kwenye umbali ambao Korea Kaskazini inaweza kuyashambulia.

0 Comments:

Post a Comment