Imeandaliwa na Staff , Grace Macha
(ni kuhusu kesi inayomkabili mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha Lengai ole Sabaya ya kujifanya mtumishi wa idara ya usalama wa Taifa (TISS) ili kujipatia chakula katika hoteli ya kimataifa jijini Arusha)
Picha ya December 14, 2016 ikimuonesha Mwenyekiti UVCCM - Arusha. Ndg. Lengai ole Sabaya. mara alipoachiwa na mahakama mwaka jana |
Mvutano mkali umeibuka baada ya upande wa Jamhuri kutaka kuliondoa mahakamani shauri la kujifanya mtumishi wa umma idara ya usalama wa Taifa (TISS) na kujipatia chakula hotel ya Kimataifa jijini Arusha, linalomkabili Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, (UV CCM), Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya.
Wakili wa Serikali, Grace Madikenya aliwasilisha ombi hilo jana
mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha, Gwantwa Mwakuga, ambapo
alieleza sababu za kufikia hatua hiyo ni shahidi wao muhimu kuwa nje ya nchi
kwa miezi 18 hivyo hataweza kufika mbele ya mahakama hiyo.
Alidai kuwa walifikia uamuzi huo kwa nia njema kabisa baada ya
kuona kuwa kuendelea kumsubiri shahidi huyo kwa kipindi hicho ni kumtesa
mshitakiwa.
Wakili wa Ole Sabaya ambaye pia ni diwani wa kata ya Sambasha,
Edna Haraka alipinga vikali ombi hilo na kuiomba mahakama hiyo iendelee na
shauri hilo huku akidai kuwa upande wa Jamhuri unaitumia Mahakama kama kichaka
cha kumnyanyasa kwa kumnyima haki mteja wao.
Alidai kuwa hii ni mara ya pili kwa upande wa jamhuri kuomba
kumfutia mashitaka mteja wake ambapo kwa mara ya kwanza walikubali mahakama
ikamfutia mashitaka lakini alikamatwa tena muda mfupi mara baada ya
kutoka kwenye chumba cha mahakama ambapo polisi walimshikilia huku wakimnyima
dhamana.
“Sasa leo tupo katika kusikiliza shahidi wa tatu na badala ya kuleta shahidi walileta maelezo ya shahidi na leo wanakuja na stori ya
kuiondoa ili waendelee kumnyanyasa mteja wetu, hapana, ofisi ya mwanasheria mkuu inatumika vibaya kwa kivuli cha Mahakama,” alisema Wakili Haraka.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Gwantwa
Mwakuga aliahirisha shauri hilo mpaka Aprili 28, mwaka huu,atakapotoa uamuzi wa
kukubali au kukataa shauri hilo kuondolewa mahakamani.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mnamo mei 18 , mwaka jana,
katika hotel ya Sky Motel, Ole Sabaya, alijifanya ni mtumishi wa
TISS na kupata huduma ya kulala katika hotel hiyo huku akihudumiwa chakula
na vinywaji wakati sio kweli.
Katika shitaka la pili, Ole Sabaya ambaye kwa sasa amesimamishwa
uongozi kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti wa mkoa wa UV CCM, anadaiwa kugushi
kitambulisho cha utumishi wa TISS kilichosomeka MT.86117 wakati akijua
kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Sabaya alikana mashitaka hayo na yuko nje kwa dhamana aliyotakiwa
kuwa na wadhamini wawili wenye mali ya shilingi milioni 10 .
ALIVYOFUTIWA MASHITAKA DESEMBA 15, MWAKA JANA
Mahakama hiyo ilimfutia mashtaka kama hayo Ole Sabaya Desemba 15,
mwaka jana baada ya Wakili wa Serikali, Grace Madikenga, kuieleza
mahakama hiyo mbele ya Hakimu Gwantwa Mwankuga, kuwa shauri hilo
lilikuwa limepangwa kuanza kusikilizwa ila jamhuri hawana nia ya
kuendelea nalo huku akitumia kifungu cha 91(1) cha sheria ya uendeshaji wa
madhauri ya jinai (CPA) kuliondoa shauri hilo mahakamani hapo.
Kitambulisho feki alichotumia mtuhumiwa Lengai Ole Sabaya |
Katika kesi hiyo Ole Sabaya, alikuwa anakabiliwa na makosa miwili
ikiwemo kughushi nyaraka za kitambulisho cha usalama wa Taifa
chenye picha yake na kutumia namba Saturday. Code. Eagle 3 idara ya usalama wa
Taifa chenye namba MT. 86117.
Hata hivyo wakati wakili wa Serikali aliomba kuondoa shauri hilo,
wakati tayari shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Inspekta Rogathe wa
Kituo cha Polisi Arusha alikuwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi
wake.
Hakimu Gwantwa alikubaliana na maombi hayo hivyo alimuachia
huru, Ole Sabaya.
Mara baada ya Mahakama kumuachia huru Ole Sabaya , polisi
walimkata tena wakati akitoka mahakamani hapo ambapo walimpakia kwenye
na gari la polisi lililokuwa na namba za usajili T 953 CSZ na
kuondoka naye.
Mtandao huu ilimtafuta Kamanda wa Polisi mkoani hapa, (RPC),
Charles Mkumbo ambapo alithibitisha jeshi hilo kumkamata tena ole Sabaya ambaye
alidai watamrejesha tena mahakamani kwa tuhuma hizohizo alizofutiwa.
"Ni kweli tumemkamata, hizo ni "technicalities" tu
za kisheria, wamemkamata watafanya taratibu za kisheria watamrudisha tena
mahakamani kwa mashtaka hayohayo," alisema kamanda huyo wakati akiongea na
mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.
No comments:
Post a Comment