Wednesday, March 26, 2014

KENYATTA ATAKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZIUNGANE KUKABILIANA NA MAJANGILI


 

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta amezitaka nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuungana pamoja katika kukabiliana na ujangili wa wanyamapori unaotishia sekta ya utalii.

 

Aidha ametaka nchi hizo kutumia rasilimali zilizopo kupambana na umasikini kwa kujijengea uwezo kiuchumi sanjari na kujenga viwanda vitakavyotoa ajira kwa wananchi huku vikiwawezesha kuingia kwenye ushindani wa kibiashara na Mataifa mengine.

 

Kenyata aliyasema hayo jana akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuongea kwenye bunge la Afrika Mashariki, (EALA) pamoja na wafanyakazi wa jumuiya hiyo kwenye ziara yake ya siku mbili aliyofanya kwenye makao hayo makuu ya jumuiya hiyo.

 

Alisema kuwa ni vema ukawepo mkakati madhubuti wa kukabiliana na wawindaji haramu wa wanyamapori, (majangili)  kwa kuhakikisha vikosi vya ulinzi wa wanyamapori  toka nchi wanachama  vinafanya kazi kwa pamoja.

 

“Watu wengi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki wanategemea utalii katika kujipatia kipato na kuna baadhi ya nchi zinapata mapato kwa asilimia kubwa kutokana na utalii. Hivyo sisi tuna wajibu wa kuhakikisha tunaweka mikakati ya kuwadhibiti hawa wawindaji haramu wanaohatarisha usalama wa urithi huu wa asili wa ukanda huu,” alisema Kenyatta.

 

Rais huyo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Marais wa EAC, alisema kuwa nchi za wanachama hazina budi kuweka nguvu pamoja kukabiliana na magaidi ili kuhakikisha wanachi wanakuwa salama huku akisisitiza kuwa huwezi kuwa salama kama kwa jirani si salama.

Akizungumzia mtengamano wa wananchi wa jumuiya hiyo alisema unazidi kuimarika ambapo kwa sasa baadhi ya nchi zinatumia vitambulisho kuvuka mipaka ingawa  Tanzania bado hawajakamilisha utoaji wa vitambulisho kwa wananchi wake ambapo wakikamilisha nao wataweza kuzunguka kwenye nchi wanachama bila kutumia hati za kusafiria.

 

Hata hivyo alisema kuwa shirikisho la kisiasa la jumuiya hiyo ni mchakato ambao unapaswa kufanyika kwa umakini na si tukio hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu huku akielezea changamoto ya urasimu uliopo katika kutekeleza  baadhi ya makubaliano waliyofikia ikiwemo yale ya upitishaji wa bidhaa miongoni mwa nchi wanachama.

 

 Rais Kenyatta alikuja nchini kwa njia ya barabara ambapo aliingilia mpaka wa Namanga mkoani Arusha ambapo aliondoka jana mchana kwa njia ya barabara akitarajiwa kupitia Rombo mkoani Kilimanjaro kwenye mpaka wa holili unaopakana na ule wa Taveta  upande wa Kenya.


No comments:

Post a Comment