Wednesday, March 26, 2014

KENYATTA AFANYA KIJIHADA KUMNUSURU SPIKA EALA KUNG'OLEWA



 

MWENYEKITI wa Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uhuru Kenyatta jana alilamizimika kufanya kikao cha dharura na wenyeviti wa wabunge toka nchi tano zinazounda jumuiya hiyo kwa kile kilichodaiwa ni kujaribu kutuliza harakati za wabunge hao kutaka kumng’oa Spika, Dk.Magareth Banbtonbg Zziwa.

Kikao hicho ambacho hakikuwa kwenye ratiba iliyotolewa asubuhi kilifanyika mara baada ya Rais Kenyatta kumaliza kuongea na waandishi ambapo muda huo alitakiwa kushiriki chakula cha mchana na wabunge wa EALA.

 

Kikao hicho kilichofanyikia kwenye ofisi ya spika kilidumu kwa dakika 40 ambapo alipomaliza alitoka na kuwapungia mkono wabunge na wafanyakazi wa jumuiya hiyo na kuondoka huku wabunge wa EALA waliokuwa eneo hilo wakionekana kuweka mkakati wa pamoja kuhakikisha hawabadilishi msimamo wa kumng’oa spika huyo kwenye mkutano wa bunge unaofanyika leo (jumatano) saa 8:30 mchana.

 

Mmoja wa wajumbe hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa wana mambo matano ya msingi yanayowafanya wafikie uamuzi wa kumng’oa spika Zziwa ambaye ameonekana kupwaya kwenye nafasi hiyo hali inayokifanya na chombo hicho kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Alisema kuwa spika huyo amekuwa akijijengea sifa binafsi kwa wakuu wa nchi hivyo kukifanya chombo hicho kuwa dhaifu katika kupigania na kusimamia ipasavyo masuala yenye maslahi kwa wananchi wote wa EAC.

 

“Kumekuwa na operesheni Kimbunga imeendeshwa Tanzania wananchi wamenyanyaswa bunge liko kimya, Rwanda, Kenya na Uganda wamevunja mkataba uliounda EAC kwa kuzitenga Tanzania na Rwanda kwenye utekelezaji wa miradi lakini bunge hili halijafanya chochote wala kukemea,” alisema mjumbe huyo.

 

Alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu za bunge hilo Spika ndiye mwenye uamuzi wa mwisho endapo hoja ya mbunge ijadiliwe au la jambo alilodai kuwa hutumia upungufu huo wa kanuni kutupa hoja hizo.

 

Aidha wabunge hao wanadai ni lazima wamng’oe spika huyo kwa madai kuwa anatumia vibaya fedha za EALA ikiwemo katika mkutano wa Chama cha Global Parlimentary for Habitat ambao yeye ni Mwenyekiti, mkutano uliofanyika Arusha Agosti. 2013.

Spika Magareth anadaiwa  kuingiza ndugu zake kwenye michezo ya wabunge wa EALA ilifanyika nchini Uganda  ambapo wanadaiwa kucheza  mpira wa pete netball  na kulipwa  Dola za Marekani 3,600 kila mmoja ingawa hawakutaja idadi yao hatua ambayo ni kinyume na utaratibu wa michezo hiyo ambayo huwashirikisha wabunge.

 

Wabunge hao wanadai kuwa Spika huyo  anasafiri sana huku  akipanga safari za kikazi kwa upendeleo kwa baadhi ya wabunge na kuwaacha wengine kwa kile walichoeleza kuwa wapo wabunge waliosafiri zaidi ya mara nne  wakati wengine hawajahi kupangiwa hata safari moja.

 Wakizungumzia hatua ya Rais Kenyatta kujaribu kumnusuru wabunge hao walisema kuwa haitawezekana na hawaamini kiongozi huyo anaweza kuwaagiza wabunge nini cha kufanya.


"Kenyatta ni mwasiasa anajua madhara ya kujaribu kuelekeza watu waliochaguliwa kwa kura, ikitokea atafanya kosa la kuelekeza asing'olewe basi atakuwa ameturahisishia zoezi la kumng'oa spika (Zziwa) amchukue akafanye naye kazi kama anamuona anafaa," alisema mmoja wa wabunge hao.


Juhudi za Tanzania Daima kumpata Spika Zziwa kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba baada ya maafisa wa ulinzi waliokuwa eneo hilo kuwazuia wandishi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment