UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti na
MACHI 2014 ________________
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba,
1. Kwa mujibu wa kifungu 20 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 na
Tangazo la Serikali Na. 30 la tarehe 14 Februari, 2014, naomba kuwasilisha
Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba. Rasimu ya Katiba
ninayoiwasilisha imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya
kukamilisha kazi ya kuratibu, kukusanya, kuchambua na kutathmini maoni ya
wananchi kuhusu Katiba Mpya.
2. Mwanzo kabisa, nieleze kwamba, Maelezo haya ninayoyatoa, ni sehemu ya
Randama (Memorandum) iliyoandaliwa na Tume kwa lengo la kufafanua kwa kina,
maudhui ya kila Ibara iliyomo katika Rasimu ya Katiba na sababu za mapendekezo
ya Ibara hizo. Hivyo, naomba maelezo yote yaliyomo katika Randama yawe
sehemu ya maelezo yangu na yaingizwe katika kumbukumbu za Bunge hili.
3. Rasimu ya Katiba ni miongoni mwa Nyaraka zilizoambatanishwa katika Ripoti
ya Tume kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania tuliyowakabidhi Waheshimiwa Marais tarehe 30 Desemba, 2013.
Nyaraka nyingine ni:
(a) Taarifa ya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba. Taarifa hii ina maoni ya Wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kikatiba ambayo ndio msingi wa uandishi wa Rasimu ya Katiba;
(b) Taarifa ya Mabaraza ya Katiba ambayo inaainisha maoni ya Wananchi kuhusu Ibara zilizokuwemo katika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba na jinsi zilivyofanyiwa kazi;
(c) Taarifa ya maoni ya Wananchi kuhusu Sera, Sheria na Utekelezaji. Taarifa hii ina maoni ya wananchi kuhusu mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa uamuzi wa kisera, kutunga au kurekebisha sheria zilizopo au utekelezaji wa kiutendaji;
(d) Taarifa ya Utafiti Kuhusu Masuala Mbalimbali ya Kikatiba, ambayo ina taarifa nne ambazo ni:
(i) Utafiti Kuhusu Madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(ii) Utafiti Kuhusu Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji;
(iii) Utafiti Kuhusu Masuala Yanayohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar; na
(iv) Ushauri Elekezi Kuhusu Mifumo ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi, Tanzania (Final Report on the Review of Various Aspects of Electoral Systems and the Electoral Commission in Tanzania).
(e) Taarifa ya Takwimu za Ukusanyaji wa maoni ya Wananchi ambayo inaainisha maeneo makuu yaliyotolewa maoni, jinsi, elimu na kazi za watoaji maoni; na
(f) Viambatisho vya Ripoti ambavyo vinaainisha hatua mbalimbali za mchakato, uamuzi, hotuba za viongozi na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Tume.
4. Ripoti ya Tume na baadhi ya Taarifa zimegawiwa kwa kila Mjumbe na Taarifa nyingine zimewekwa katika Maktaba ya Bunge ili kuwawezesha Wajumbe kufanya marejeo. Tume inaamini kwamba Ripoti na Taarifa zinazowasilishwa pamoja na maelezo haya zitawasaidia Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kujadili na kufanya uamuzi sahihi kwa kila Ibara iliyopendekezwa kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na Taifa kwa jumla.
Shukrani kwa Uteuzi na Kuchaguliwa
Mheshimiwa Mwenyekiti,
5. Naomba kutumia fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha
Tume kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba na kuiwasilisha katika Bunge
lako.
6. Mwenyezi Mungu alitulinda katika mchakato mzima wa kuratibu na kukusanya
maoni ya wananchi hadi kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu. Kwa huzuni kubwa
tulimpoteza mmoja wetu, Dkt. Adrian Sengondo Mvungi katika hatua za mwisho za
kazi yetu. Mchango wa Dkt. Mvungi ulikuwa mkubwa sana na ingawa hatuko
naye, Rasimu ya Katiba ninayoiwasilisha imesheheni maoni yake mengi. Kazi ya
Mungu haina makosa na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake
mahali pema peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
7. Napenda kukupongeza wewe mwenyewe na Makamu wako kwa kuchaguliwa
kwenu ili kuongoza Bunge hili ambalo lina jukumu kubwa la kujadili na kupitisha
masharti ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Bunge hili
Maalum la Katiba litapendekeza Katiba Mpya itakayopigiwa kura ya maoni na
wananchi. Kuchaguliwa kwenu ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wajumbe wa
Bunge Maalum juu yenu. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awawezeshe
kuifanya kazi hiyo kwa weledi, hekima, busara, uzalendo na uadilifu mkubwa ili
kukamilisha jukumu la Bunge Maalum la Katiba. Tunawapongeza pia wajumbe
wote wa Bunge Maalum la Katiba na tunawatakia kila la kheri katika kutimiza
jukumu ambalo taifa limewakabidhi.
Shukrani kwa Marais, Watendaji
Mheshimiwa Mwenyekiti,
8. Kwa niaba ya Wajumbe, na Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kwa niaba yangu mwenyewe, ninawashukuru kwa dhati kabisa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohammed Shein, kwa mambo yafuatayo:
Kwanza, kwa uamuzi wao wa busara wa kusikiliza matakwa ya Wananchi
ya kutaka Katiba Mpya.
Pili, kwa kututeua kuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kutuwezesha kuifanya na kuikamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba
kwa wakati uliowekwa kisheria.
Tatu, kwa kuipatia Tume, Watumishi wa Sekretarieti walio makini, wenye
ujuzi, utaalamu na uelewa katika fani zao walioiwezesha Tume kukamilisha
kazi yake kwa ufanisi.
Nne kuheshimu, kuisimamia na kuipa Tume nyenzo za kutekeleza
majukumu yake kwa uwazi na bila ya kuiingilia.
Mwisho kwa mujibu wa sheria, kuunda Bunge Maalum la Katiba lililojaa
wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali ya jamii za watanzania.
9. Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Mawaziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
Wanasheria Wakuu wa Serikali; Makatibu Wakuu Viongozi, Watendaji Wakuu wa
Wizara za Katiba na Sheria; Wakuu wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Wakurugenzi na
Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Watendaji wa Tarafa, Kata, Shehia,
Vijiji na Mitaa kwa ushirikiano mzuri waliotoa kwa Tume wakati wote wa mchakato
wa kupata maoni ya wananchi.
10.Tume pia inatoa shukrani maalum kwa Jeshi la Polisi la Tanzania na vyombo
vingine vya Ulinzi na Usalama kwa kuhakikisha mchakato mzima unaenda kwa
usalama. Aidha, Tume inatoa shukrani kwa Vyama vya Siasa, Jumuiya za Kidini,
Asasi za Kiraia, Vyombo vya Habari, Taasisi na Makundi mengine kwa mchango
wao mkubwa wakati wote wa mchakato wa kupata maoni ya wananchi kuhusu
Katiba Mpya.
Shukrani kwa Wananchi
Mheshimiwa Mwenyekiti,
11.Kwa namna na kwa uzito wa pekee, Tume inawashukuru sana Wananchi wote
kwa ushiriki, na kwa mchango wao mkubwa wa mawazo, maoni na mapendekezo
yaliyowezesha kupatikana kwa Rasimu ya Katiba. Hii ni mara ya kwanza katika
historia ya nchi yetu, kwa wananchi wa kawaida kushiriki katika kutoa maoni kwa
uhuru na uwazi kuhusu aina ya katiba wanayoitaka, na wamefanya hivyo kwa
wingi, uhuru, uwazi, umakini na kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
12.Baada ya kutoa shukrani sasa naomba nitoe maelezo marefu kidogo kuhusu
Rasimu ya Katiba. Maeneo yote ya Rasimu ni muhimu lakini kwanza
nitayazungumzia machache kwa ujumla kutokana na umuhimu wake. Baadaye
nitaizungumzia Rasimu ya Katiba kwa kupitia maudhui ya kila Sura. Maelezo kwa
kina ya kila Ibara na sababu za mapendekezo zinaelezwa kwenye Randama
ambayo tayari imekabidhiwa kwa Katibu wa Bunge Maalum la Katiba na wabunge
wote watapata nakala.
Dhana ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti,
13.Katika nchi yoyote, msingi wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba. Katiba ni
sheria kuu au sheria mama katika nchi yoyote. Sheria nyingine zote zinategemea
au zinatungwa kwa mujibu wa Katiba. Wakati mwingine Katiba hutafsiriwa kuwa
ni mkataba wa Kijamii kati ya Viongozi na Wananchi. Ni makubaliano ya wananchi
kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao.
Katiba ni muafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya kuendesha nchi.
14.Katiba ni Sheria ya msingi ambayo inaweka mfumo wa uendeshaji wa nchi. Katiba
inafanya hivyo kwa kuainisha misingi ya taifa, mgawanyo wa madaraka na
majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi wake, mgawanyo na ukomo wa
mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
15.Katika nchi ambazo zimefanya mabadiliko ya katiba, njia kuu zifuatazo huwa
zinatumika:
(i) Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya kikatiba;
(ii) Kuundwa Tume ya kuandaa Katiba kwa kupitia sheria zilizopo; na
(iii) Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya Katiba.
16.Nchi yetu imetumia utaratibu wa Bunge kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Sura ya 83, inayoelezea utaratibu wa mchakato mzima wa kupata katiba mpya
ambao unawashirikisha wananchi kisheria katika hatua zote muhimu za uandikaji
wa katiba yao.
17.Sheria imeanzisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ikaweka Hadidu za Rejea na
kuipa Tume jukumu la kuratibu, kukusanya maoni ya wananchi, kuchambua na
kutathmini maoni na kuandaa Ripoti na Rasimu ya Katiba. Baadaye wananchi,
kupitia Mabaraza ya Katiba, walipewa fursa tena ya kutoa maoni yao kabla ya
Tume kufanya maboresho na kuiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba; hatua
ambayo ndipo tulipofikia hivi sasa.
18.Baada ya Bunge Maalum kutoa Katiba inayopendekezwa, wananchi watapata fursa
ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba Mpya kupitia kura ya maoni. Si nia
yangu kutoa maelezo kuhusu historia ya katiba nchini, kwa kuonyesha tumetoka
wapi, tupo wapi na tunakwenda wapi. Maelezo ya kina kuhusu suala hilo yamo
kwenye Sura ya Tatu ya Ripoti ya Tume kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Utangulizi wa Rasimu ya Katiba
19.Rasimu ya Katiba inaanza na utangulizi. Utangulizi ni sehemu muhimu ya Katiba ya
nchi. Katika hali ya sasa ya mwelekeo wa taaluma ya sheria duniani, na kwa
mujibu wa Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 ya Sheria za Tanzania, Utangulizi
ni sehemu ya Katiba. Utangulizi ndio kioo kinachoonyesha dhamira ya Katiba kwa
kutoa tafsiri ya jumla ya Katiba. Sehemu hii inatoa taswira na picha halisi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake, historia yao, matarajio yao,
misingi na masuala muhimu ambayo wanataka kuyaendeleza katika jamii, kizazi
hadi kizazi.
20.Utangulizi wa Rasimu ya Katiba unatamka rasmi kwamba Katiba hii ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imetungwa na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kuthibitishwa na wananchi kupitia kura ya maoni.
Eneo la Jamhuri
21.Tume imependekeza eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lijumuishe eneo
lote la iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika ikijumuisha sehemu yake ya bahari na
eneo lote la iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya
bahari, kama ilivyoainishwa katika Katiba za Uhuru za nchi mbili hizi.
22.Madhumuni ya kubainisha eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
kukubaliana na maoni ya wananchi waliotaka kuwepo kwa ufafanuzi thabiti kuhusu
eneo na mipaka ya nchi. Kufanya hivi, kutatunza historia ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kuondoa utata na hisia kwamba mipaka ya nchi hizi mbili
inabadilika.
23.Lengo pia la sehemu hii ni kuainisha mipaka ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inayotambulika na mikataba mbalimbali ya kimataifa na Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Bahari wa mwaka 1982.
Misingi Mikuu ya Taifa
24.Rasimu ya Katiba, kama ilivyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977, imeorodhesha misingi mikuu ya Taifa inayojenga Taifa la
Tanzania na kusimamia ustawi wa wananchi wake. Katiba ya sasa ina misingi
mikuu minne, yaani, uhuru, haki, udugu na amani. Wananchi walipendekeza
misingi mingine minne iongezwe, yaani utu, usawa, umoja na mshikamano. Kwa
hiyo, misingi inayopendekezwa ni Utu, Uhuru, Haki, Udugu, Amani, Usawa, Umoja
na Mshikamano.
Tunu za Taifa
25.Tunu za Taifa ni mambo muhimu ya kujivunia kwa jamii yoyote ile. Tunu ndio
msingi wa maadili na utamaduni wa jamii. Tume inapendekeza tunu zifuatazo
zitajwe ndani ya Katiba: Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na
Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa.
26.Madhumuni ya kupendekeza Tunu hizi kuingizwa katika Katiba ni kuheshimu na
kuzingatia maoni na mapendekezo ya wananchi kuwa Katiba itaje Tunu za Taifa ili
kuifanya jamii kuzitambua, kuzithamini na kuzitekeleza.
Malengo Muhimu
27.Sura ya Pili ya Rasimu inaelezea Malengo Muhimu na Misingi ya Shughuli za
Serikali na Sera za Kitaifa. Wakati wa kukusanya maoni, wananchi wengi, hasa
wale wanaoishi vijijini, walizungumzia sana dira ya taifa kuhusu maendeleo yao.
Misingi Mikuu ya Taifa
24.Rasimu ya Katiba, kama ilivyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977, imeorodhesha misingi mikuu ya Taifa inayojenga Taifa la
Tanzania na kusimamia ustawi wa wananchi wake. Katiba ya sasa ina misingi
mikuu minne, yaani, uhuru, haki, udugu na amani. Wananchi walipendekeza
misingi mingine minne iongezwe, yaani utu, usawa, umoja na mshikamano. Kwa
hiyo, misingi inayopendekezwa ni Utu, Uhuru, Haki, Udugu, Amani, Usawa, Umoja
na Mshikamano.
Tunu za Taifa
25.Tunu za Taifa ni mambo muhimu ya kujivunia kwa jamii yoyote ile. Tunu ndio
msingi wa maadili na utamaduni wa jamii. Tume inapendekeza tunu zifuatazo
zitajwe ndani ya Katiba: Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na
Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa.
26.Madhumuni ya kupendekeza Tunu hizi kuingizwa katika Katiba ni kuheshimu na
kuzingatia maoni na mapendekezo ya wananchi kuwa Katiba itaje Tunu za Taifa ili
kuifanya jamii kuzitambua, kuzithamini na kuzitekeleza.
Malengo Muhimu
27.Sura ya Pili ya Rasimu inaelezea Malengo Muhimu na Misingi ya Shughuli za
Serikali na Sera za Kitaifa. Wakati wa kukusanya maoni, wananchi wengi, hasa
wale wanaoishi vijijini, walizungumzia sana dira ya taifa kuhusu maendeleo yao.
28.Moja ya mambo ambayo wananchi waliyatolea maoni kwa msisitizo mkubwa ni
ardhi. Wananchi wengi walilalamika kwamba wanayo matatizo kutokana na
ugumu wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine lakini wawekezaji
wakubwa wanapewa upendeleo wa kupata ardhi kwa urahisi. Pia, kuna
migongano isiyokwisha ya makundi mbalimbali, wakulima na wafugaji, wananchi
na mamlaka za hifadhi za taifa na kadhalika. Kuna malalamiko mengi kuhusu
huduma za kilimo kama vile zana za kilimo, pembejeo na mizania ya bei.
29.Mkulima mmoja wa pamba, wilaya ya Kahama, alilalamika kwamba ingawa
wanaambiwa na Serikali kwamba watajiondoa kwenye lindi la umaskini kupitia
kilimo bora, lakini haoni dalili hizo. Alisema wakulima wana matatizo ya mbegu,
dawa za kuuwa wadudu na bei ndogo ya mazao. Alisema mwaka 2012 alikuwa
ametumia shilingi mia nane kupata kilo moja ya pamba, lakini bei aliyopewa
ilikuwa shilingi mia sita. Katika mazingira haya, badala ya kupata maisha bora,
anazidi kuwa maskini.
30.Wakulima wa mazao ya chakula wana matatizo ya aina hiyo, na hivyo hivyo kwa
wakulima wa mazao ya biashara. Wafugaji nao wana matatizo ya ardhi ya
malisho, maji, madawa ya mifugo na bei ya mifugo yao. Wavuvi wana matatizo ya
maeneo ya uvuvi, zana za uvuvi bei na kadhalika.
31.Wananchi pia walizumgumzia hifadhi ya jamii, hasa kwa wazee. Wanasema
wafanyakazi wana mifumo ya hifadhi ya jamii na mishahara yao inaongezwa kila
wakati. Kwa Wakulima, mapato yao ni madogo na wakizeeka hawana hifadhi
yoyote. Hata matibabu ya wazee siyo bure kama utaratibu wa Serikali unavyoelekeza, kwani sharti wanunue dawa wakati uwezo wao wa kifedha ni
mdogo.
32.Wananchi pia walizungumzia elimu na huduma za afya. Kwa maoni yao, elimu
bora na huduma za afya bora zinatolewa kwa watu wa tabaka la juu. Wao
wanabaki na shule zenye huduma hafifu na zahanati zenye kutoa huduma hafifu.
33.Tume imezingatia maoni ya wananchi na imependekeza mambo kadhaa. Kubwa ni
kuweka dira ya taifa. Sura ya Pili yote ya Rasimu ya Katiba inazungumzia dira ya
taifa. Madhumuni ya kuweka Malengo Muhimu na Misingi ya Shughuli za Serikali
ni kuhakikisha kuwa Serikali na mamlaka zake zinapewa mwongozo wa kisera na
mwelekeo wa kiutendaji. Pamoja na mambo mengine malengo yafuatayo
yamewekwa kwa ajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi:
(i) Kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo
vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi;
(ii) Kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa
kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na
nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao;
(iii) Kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji
na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya mazao yao;
(iv) Kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji wa mizania ya bei za
mazao na pembejeo.
34.Haki ya kumiliki mali imejumuishwa kwenye haki za binadamu, na vivyo hivyo, haki
ya elimu bora ya msingi ipatikanayo bila malipo.
Nimeishia ukurasa wa 11 nitawaletea hutuba nyingine baadae kidogo, hutuba hii inakurasa 65... someni....na mpitie rasimu.
0 Comments:
Post a Comment