Shughuli hizo zilizowakutanisha wahanga 40, viongozi na wanachama wa chama hicho zilifanyika kwenye ofisi za wilaya ya Arusha za chama hicho zilizopo Ngarenaro.
Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Ephata Nanyaro na Katibu wake, Martn Sarungi waliwagawia wahanga hao vitu mbalimbali vilivyotolewa na wanachama na wapenzi wa chama hicho ikiwemo fedha taslim, Sabuni, unga, mchele, matunda na vyakula mbalimbali
Zoezi hilo la kupokea misaada na kuigawa kwa waathirika hao litadumu kwa wiki moja kuanzia januari 4 mpaka 11 mwaka huu ambapo wahanga hao 39 ni kutoka jiji la Arusha huku mmoja akitokea wilayani Arumeru ambaye ni mjane wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo aliyefariki kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni
Wahanga hao ambao ni wale walipoteza ndugu zao, waliumizwa maeneo mbalimbali ya mwili na hivyo kupata ulemavu wa kudumu siku ya maandamano na mkutano wa chama hicho wa janiari 5, 2011 ambapo polisi waliwauwa kwa risasi watu watatu Juma Ismail, Denis Shirima na mmoja wa Kenya huku wananchi wengine kadhaa kujeruhiwa.
Wahanga wengine ni wale wa tukio la June 15, mwaka jana ambapo bomu ambalo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alidai lilirushwa na polisi kwenye viwanja vya Soweto wakati akifunga mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata nne za Arusha ambapo walifariki watu watano akiwemo Katibu wa Chadema Kata ya Sokon1, Judith Mollel ambapo wengine kadhaa walijeruhiwa.
Aidha wahanga wengine ni wale waliojeruhiwa Juni 18, mwaka jana wakati walipokusanyika kwenye viwanja vya Soweto kwa lengo la kuagaa miili ya wenzao waliuwawa June 15 ambapo polisi waliwatawanya wananchi hao bila kutoa taarifa ya onyo ya kuwataka kutawanyika ambapo viongozi kadhaa wa chama hicho walikamatwa na kufikishwa polisi lakini hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi yao.
WAHANGA WANENA
Rafael Amosi anasema kwa sasa anaishi maisha magumu baada
ya kupata ulemavu wa kudumu kwani mkono wake wa kushoto umepinda na haunyooki huku
mkono wake wa kulia akiwa hawezi kuuzungusha kutokana na kujeruhiwa vibaya
kwenye bega.
Anasema kuwa siku ya juni 18 mwaka jana alikuwa ni miongoni
mwa wananchi wa Arusha walijitokeza kwa ajili ya kwenda kuaga miili ya wananchi
wanne waliofariki kwa kupigwa mabomu na risasi za moto kwenye mkutano wa
kufunga kampeni za Chadema kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata
nne.
Amos anasema akiwa anasikiliza viongozi wa Chadema
wakiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na wabunge wakiongea alishtushwa na milio ya mabomu ya
machozi na maji ya kuwasha yaliyokuwa yanarushwa na polisi ambapo alihamaki na
kuanza kukimbia.
“Kabla sijafika mbali nilianguka ambapo kutokana na watu
kukimbia hovyo kila mmoja akijaribu kuokoa maisha yake walikuwa wakinikanyaga
pale chini nilipokuwa, nilipata maumivu makali mpaka nikapoteza fahamu”
“Nilizinduka nikakuta nimezunukwa na kundi la polisi wenye
virungu ambapo nilipokuwa nikijaribu kusimama nilishindwa baadaye nikabaini kuwa
nimevunjika mguu wa kushoto kutokana na kukanyagwa na watu, hapo sasa polisi
wakaendelea kunishambulia kwa virungu.”
“Huu mkono wa kushoto na bega la kulia vilivunjika wakati
nikijitahidi kujikinga virungu vya polisi visinipate usoni kwa kweli
nilisikitika sana kwani polisi badala ya kunisaidia wao ndiyo waliniumiza zaidi.”
Anaeleza Rafael kwa masikitiko.
Anasema kuwa kwa sasa yeye hana ajira kwani taxi aliyokuwa
akiendesha alikua ameajiriwa tu hivyo kutokana na ulemavu alio nao hawezi
kufanya kazi hiyo tena. Anaomba msaada wa fedha walau aweze kulipia watoto wake
ada ya shule ingawa alisema kuwa bado anaamini mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa
na kijamii yatapatikana kupitia Chadema.
Sagida Rajab (30)
Anaongea huku machozi ya uchungu yakitiririka machoni
pake, anasema kuwa tukio la juni 15, mwaka jana ni gumu sana kwake kwani
limesababisha maisha yake yabadilike kabisa na kuemsababisha sasa awe mjane.
Anasema siku hiyo ilikuwa mbaya kwake kwani alimpoteza
mwanaye Fahad Jamal, (7) aliyekuwa darasa la kwanza ambaye alifariki baada ya
kujeruhiwa vibaya kwa risasi huku mwanae mwingine Abuu Adam, (10) akijeruhiwa
vibaya hali iliyomsababisha akatwe mguu wake wa kulia hivyo kwa sasa ni ulemavu
wa kudumu.
“Mume wangu, Adam Kareem amefariki dunia oktoba 25, mwaka
jana kutokana na kuzidiwa na shinikizo la damu. Alikuwa akiwaza sana juu ya
tukio hilo lililosababisha kifo cha mtoto wetu na mwingine kuwa mlemavu”
anasema Sagida huku akiendelea kulia hali iliyosababisha watu wengine walikuwa
wakimsikiliza nao kulia.
Anaelezea namna
watoto wake walivyokumbwa na kadhia hiyo Juni 15, mwaka jana wakati wakitoka madras ambapo walikuwa
wanapita eneo karibu na mzunguko wa magari uliopo karibu na viwanja vya Soweto.
Anasema kuwa watoto wake hao walijeruhiwa vibaya kwa risasi ambapo Fahad alifariki dunia na Abuu
mpaka sasa anendelea na matibabu akiwa amekatwa mguu wake wa kulia alipigwa
risasi ikatokea upande wapili.
Sagida anasema kwa sasa hali yake kiafya si nzuri kwani
tukio hilo limemchanganya sana akili na anaomba Chadema na Serikali waangalie namna ya kumsaidia kwani yeye
ni mama wa nyumbani alikuwa anamtegemea mume wake ambaye naye kafariki hivyo anahitaji asaidiwe ili
aweze kumhudumia mtoto wake ambaye ni mlemavu kwa sasa.
Ibrahim Rashid (14) mkazi wa Mianzini ambaye wakati wa
tukio alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Levelos anasimulia namna
alivyojeruhiwa kwa risasi kwenye mkutano wa Chadema uliofanyika kwenye viwanja
vya Soweto, juni 15, mwaka jana.
Anasema mpaka sasa anatembea na risasi iliyopo maeneo
karibu na kitovu baada ya madaktari kumueleza kuwa eneo iliyopo ni hatari hivyo
inabidi asubiri mpaka ipande juu ndipo arudi hosptali waweze kuitoa.
Anasema kuwa kuna wakati akikaa anapata maumivu makali
maeneo karibu na kibofu cha mkojo kutokana na risasi hiyo ambapo risasi
nyiongine iliyokuwa kwenye paja aliitoa mwenyewe.
“Hospitali hawakunitoa risasi zote, kuna siku nilikuwa nimevaa
suruale laini nikaipandisha mpaka juu kwenye kidonda kilichopo kwenye paja
nikaondoa plasta iliyowekwa nikaona kitu kama ganda sikujua ni nini nikamwambia
dada.”
“Dada akaniambia nikifute taratibu nikakivuta mpaka
kikatoka kumbe ilikuwa ni risasi mpaka leo nimeiweka wala sijaitupa ila kwa
sasa naomba nisaidiwe kwenda kuitoa hii iliyopo hapa karibu na kitovu inaniuma
sana, baba yangu ni mzee hana fedha.” Anasema mtoto Ibrahim.
“Mimi nilikuwa napita pale kwenye njia karibu na uwanja
wa Soweto nikasikia kitu kinaniwasha hapa kwenye paja la kulia nikagusa nikaona
damu nikamkimbilia baba mmoja aliyekuwa mbele yangu nikamshika kwa nguvu”
anasema mtoto Ibrahim akielezea namna alivyokumbwa na mkasa huo.
“Nikamwambia nakufa huku nikilia nikalala chini,
akanifungua suruale akaona jeraha akanibeba akaniweka kwenye gari lake
akanikimbiza kwenye hospitali ya dkt Mohamed wakanipa huduma ya kwanza kuzuia
damu isitike nyingi wakashauri niwahishwe hospitali ya Mount Meru.”
“Tukaondoka kufika pale watu waliokuwa mapokezi wakasema
hakuna huduma wote hawa ni wa Chadema yule baba akanichukua akanipeleka
hospitali ya Selian nikapatiwa matibabu” anasema mtoto Ibrahim ambaye
aliambatana na mama yake, Buni Rashid, (30).
Anasema kuwa mbinu hizo ovu haziwezi kufanikiwa kwa kuwa Chadema wanamtegemea Mungu hivyo wataendelea kushinda jambo alilodai kuwa hata sasa licha ya matukio mengi ambayo wananchi wameuwawa na kuumizwa lakini bado wameshikamana na harakati zinaendelea.
Nanyaro ambaye pia ni diwani wa kata ya Levelos anasisitiza kuwa wataendelea kupigania uhuru wa kweli wa Taifa hili kwa lengo la kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao, kodi inayokusanywa inatumika vizuri na nchi inaongozwa kwa misingi ya utawala bora huku uwazi kwenye kila jambo ikiwemo mikataba mikubwa inayohusu rasilimali za umma ikiwekwa wazi kwa wananchi.
“Msingi wa mauaji haya yanayofanywa na vyombo vya dola ni kurudisha nyuma harakati zetu za kupigania wanyonge na kuwaamsha watu kudai haki zao, wanatumia risasi tulizonunua kwa fedha zetu wenyewe kwa kodi tunazolipa, badala ya kutulinda wanatuua lakini sisi tunawaambia haya wanayoyafanya hatukatishi tama bali yanatuongezea ari ya kupigania kuhakikisha nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala bora.” Anasisitiza Nanyaro.
MWISHO
Mhanga wa mabomu, Rafael Amaos akionyesha namna mikono yake ilivyolemaa hivyo kushindwa kuinyoosha.
MTOTO Ibrahim
Rashid (14) akionyesha eneo linalomuuma kwa sasa kutokana na risasi ambayo haijatolewa mwilini kwake ambayo iko eneo karibu na kitovu
Sagida Rajab (30) mwenye hijabu akiwa anaelezea namna mtoto wake mmoja alivyofariki na mwingine amekatwa mguu wa kulia walipopigwa risasi wakitoka madrasa hali iliyosababisha mumewe afe kwa shinikizo la damu
0 Comments:
Post a Comment