WANANCHI 43 wa Vijiji vya
Kiding`a,Moivo,Kirevi ,Sambasha na Kiranyi wilaya ya Arumeru wamesema
kuwa wapo tayari kupisha ujenzi wa barabara ya Mianzini hadi Timbolo
yenye umbali wa kilomita 8 endapo watalipwa fidia ya mali
walizoendeleza pembezoni mwa barabara hiyo zenye thamani ya zaidi ya
shilingi bilioni 3.2.
Hayo yalisemwa januari 20, mwaka huu kwa nyakati tofauti na mashahidi watano
wa upande wa waleta maombi, mbele ya jaji wa mahakama Kuu Kanda ya
Arusha, Fatma Mssengi anayesikiliza shauri la ardhi namba 18/2013
lililofunguliwa na wananchi hao.
Wakiongozwa na wakili wao, Modest Akida mashahidi hao walisema kuwa
wako tayari kubomoa nyumba zao na kupisha ujenzi wa barabara hiyo endapo
Halmashauri ya wilaya ya Arusha ambaye ndiye mdaiwa kwenye shauri hilo
itawalipa fidia stahiki kwa mujibu ya sheria ya barabara ya mwaka 2007
Shahidi wa tatu, Gideon Lukumay, (74), aliieleza mahakama hiyo kuwa
maeneo hayo wanayamiliki kwa mujibu wa sheria za kimila kwani
waliyaridhi kutoka kwa mababu ambapo barabara hiyo ilikuwa inatumika
kupitisha ng’ombe kabla ya kalasinga mmoja ambaye hakumtaja jina
kumuomba kiongozi wao chifu ili aitengeneze aweze kuitumia kupita kwa
gari kwa ajili ya kwenda kubeba magogo.
Alisema kuwa anachojua barabara hiyo ni mali ya wananchi
kwani ndiyo wamekuwa wakiikarabati kwa kipindi chote kabla halmashauri
ya wilaya ya Arusha kuanza kuikarabati.
“Baada ya nyumba
zetu kupigwa alama ya x tulipeleka malalamiko Halmashauri na kuiuliza
kuwa kwanini inataka kutuone kwa kutubomolea bila kufidiwa lakini
hatukupata majibu yanayoeleweka,binafsi ningefidiwa ningeondoka,”
alisema Lukumay.
Kwa upande wake shahidi wa kwanza, Fanuel Lamai, aliieleza
mahakama hiyo Aprili 14, mwaka jana Halmashauri walitumia katapila na
kuvunja kingo za barabara,kukata miti kwa kutumia mashine huku zoezi
hilo likifanyika chini ya uangalizi wa polisi wenye silaha huku akiweka
wazi kuwa hawapingi ujenzi wa barabara hiyo ila wanaomba kulipwa fidia.
“Nilikuwepo wakati zoezi la bomoa bomoa linaanza waliharibu uzio wa
nyumba za watu pamoja na kung’oa miti,pia niliweza kupiga picha za
mnato kama utahitaji mheshimiwa hakimu naweza kukupatia” Alisema shahidi
wa tano, Munjaya Ngarashi
Upande wa waleta maombi wamemaliza kutoa ushahidi wao ambapo ambapo
walileta mashahidi watano, wakiwemo Agnes Martin (67) na Ndeai Nembate.
Shauri
hilo limeahirishwa mpaka Januari 22, mwaka huu ambapo upande wa wadaiwa
ambao ni Halmashauri ambapo wakili wa halmashauri hiyo, Jonathan
aliieleza mahakama kuwa wanatarajiwa kuleta mashahidi wao watano.
Katika madai yao ya msingi wananchi hao 43 wanaiomba mahakama hiyo
itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa ardhi na mali zao zilizopo maeneo
ya pembezoni mwa barabara ya Mianzini mpaka Timbolo.
Pia
wanaiomba mahakama hiyo iwaelekeze halmashauri ya wilaya ya Arusha
iwalipe fidia ya ardhi waliyoiendeleza na mali zao yenye thamani ya
zaidi ya sh biloni 3.2 ili waweze kupisha ujenzi wa barabara hiyo ya
mianzini mpaka Timbolo.
Aidha wananchi hao wanadai novemba 22, 2011 walipewa notisi
ya kuondoka kwenye maeneo hayo na Halmashauri ya wilaya ya Arusha kwa
madai kuwa ni sehemu ya barabara jambo ambalo wanapingana nalo ambapo
wameiomba mahakama hiyo kuweka zuio la kudumu la wao kutoondolewa mpaka
shauri hilo liishe.
Wananchi hao wanadai kuwa wanamili maeneo hayo kihalali
kwani wengine wamerithishwa na mababu huku wengine wakiyamiliki kwa
mujibu wa sheria za mila na baadhi wameyanunua kwa wenyeji wa maeneo
hayo.
No comments:
Post a Comment