MIANZINII TOMBOLO WAGOMA KUPISHA BARABARA BILA FIDIA

WANANCHI 43 wa Vijiji vya Kiding`a,Moivo,Kirevi ,Sambasha na Kiranyi wilaya ya Arumeru wamesema kuwa wapo tayari kupisha ujenzi wa barabara ya Mianzini hadi Timbolo yenye umbali  wa kilomita 8 endapo watalipwa fidia ya mali walizoendeleza pembezoni mwa barabara hiyo zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.2.



Hayo yalisemwa januari 20, mwaka huu kwa nyakati tofauti na mashahidi watano wa upande wa waleta maombi, mbele ya jaji wa mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Fatma Mssengi  anayesikiliza shauri la ardhi namba 18/2013 lililofunguliwa na wananchi hao.

Wakiongozwa na wakili wao, Modest Akida mashahidi hao walisema kuwa wako tayari kubomoa nyumba zao na kupisha ujenzi wa barabara hiyo endapo Halmashauri ya wilaya ya Arusha ambaye ndiye mdaiwa kwenye shauri hilo itawalipa fidia stahiki kwa mujibu ya sheria ya barabara ya mwaka 2007

Shahidi wa tatu, Gideon Lukumay, (74), aliieleza mahakama hiyo kuwa maeneo hayo wanayamiliki kwa mujibu wa sheria za kimila kwani waliyaridhi kutoka kwa mababu ambapo barabara hiyo  ilikuwa inatumika kupitisha ng’ombe kabla ya kalasinga mmoja ambaye hakumtaja jina kumuomba kiongozi wao chifu ili aitengeneze aweze kuitumia kupita kwa gari kwa ajili ya kwenda kubeba magogo.



Alisema kuwa anachojua barabara hiyo ni mali ya wananchi kwani ndiyo wamekuwa wakiikarabati kwa kipindi chote kabla halmashauri ya wilaya ya Arusha kuanza kuikarabati.



“Baada ya nyumba zetu kupigwa alama ya  x tulipeleka malalamiko Halmashauri na kuiuliza kuwa kwanini inataka kutuone kwa kutubomolea bila kufidiwa lakini hatukupata majibu yanayoeleweka,binafsi ningefidiwa ningeondoka,” alisema Lukumay.



Kwa upande wake shahidi wa kwanza, Fanuel Lamai, aliieleza mahakama hiyo Aprili 14, mwaka jana Halmashauri walitumia katapila na kuvunja kingo za barabara,kukata miti kwa kutumia mashine huku zoezi hilo likifanyika chini ya uangalizi wa polisi wenye silaha huku akiweka wazi kuwa hawapingi ujenzi wa barabara hiyo ila wanaomba kulipwa fidia.

 “Nilikuwepo wakati zoezi la bomoa bomoa linaanza waliharibu uzio wa nyumba za watu pamoja na kung’oa miti,pia niliweza kupiga picha za mnato kama utahitaji mheshimiwa hakimu naweza kukupatia” Alisema shahidi wa tano, Munjaya Ngarashi

Upande wa waleta maombi wamemaliza kutoa ushahidi wao ambapo ambapo walileta mashahidi watano, wakiwemo Agnes Martin (67) na Ndeai Nembate.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka Januari 22, mwaka huu ambapo upande wa wadaiwa ambao ni Halmashauri ambapo wakili wa halmashauri hiyo, Jonathan  aliieleza mahakama kuwa  wanatarajiwa kuleta mashahidi wao watano.

Katika madai yao ya msingi wananchi hao 43 wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa ardhi na mali zao zilizopo maeneo ya pembezoni mwa barabara ya Mianzini mpaka Timbolo.

Pia wanaiomba mahakama hiyo iwaelekeze halmashauri ya wilaya ya Arusha iwalipe fidia ya ardhi waliyoiendeleza na mali zao yenye thamani ya zaidi ya sh biloni 3.2 ili waweze kupisha ujenzi wa barabara hiyo ya mianzini mpaka Timbolo.



Aidha wananchi hao wanadai novemba 22, 2011 walipewa notisi ya kuondoka kwenye maeneo hayo na Halmashauri ya wilaya ya Arusha kwa madai kuwa ni sehemu ya barabara jambo ambalo wanapingana nalo ambapo wameiomba mahakama hiyo kuweka zuio la kudumu la wao kutoondolewa mpaka shauri hilo liishe.



Wananchi hao wanadai kuwa wanamili maeneo hayo kihalali kwani wengine wamerithishwa na mababu huku wengine wakiyamiliki kwa mujibu wa sheria za mila na baadhi wameyanunua kwa wenyeji wa maeneo hayo.


0 Comments:

Post a Comment