CHADEMA ARUSHA WAKUMBUKA WAHANGA WA MABOMU

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) kimesema kuwa mbinu mbalimbali zinazofanywa na watawala  ikiwemo kuwajeruhi na kuwauwa viongozi na wanachama wao kwa mabomu na silaha za moto kwa lengo la  kurududisha nyuma harakati zao za kuwaamsha wananchi kujua haki zao na kuzidai haitafanikiwa.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Arusha, Ephata Nanyaro wakati alipokuwa akitoa msaada kwa wahanga wa matukio ya mabomu yanayodaiwa kurushwa na polisi kwenye mikutano mbalimbali ya chama hicho.

Alisema kuwa mbinu hizo ovu haiwezi kufanikiwa kwa kuwa Chadema wanamtegemea Mungu hivyo wataendelea kushinda jambo alilodai kuwa hata sasa licha ya matukio mengi ambayo wananchi wameuwawa na kuumizwa lakini bado wameshikamana na harakati zinaendelea.

Nanyaro ambaye pia ni diwani wa kata ya Levelos alisema kuwa wataendelea kupigania uhuru wa kweli wa Taifa hili kwa lengo la kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao, kodi inayokusanywa inatumika vizuri na nchi inaongozwa kwa misingi ya utawala bora huku uwazi kwenye kila jambo ikiwemo mikataba mikubwa inayohusu rasilimali za umma ikiwekwa wazi kwa wananchi.

“Msingi wa mauaji haya yanayofanywa na vyombo vya dola ni kurudisha nyuma harakati zetu za kupigania wanyonge na kuwaamsha watu kudai haki zao, wanatumia risasi tulizonunua kwa fedha zetu wenyewe kwa kodi  tunazolipa, badala ya kutulinda wanatuua lakini sisi tunawaambia haya wanayoyafanya hatukatishi tama bali yanatuongezea ari ya kupigania kuhakikisha nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala bora.” alisema Nanyaro.

Kwa upande wake Katibu wa chama hicho wilayani hapa, Martin Sarungi alisema kuwa jumla ya wahanga 40 watapatiwa vitu mbalimbali vilivyotolewa na wanachama na wapenzi wa chama hicho ikiwemo fedha taslim, Sabuni, unga, mchele, matunda na vyakula mbalimbali.

Alisema kuwa kati ya  wahanga hao 39 ni kutoka jiji la Arusha huku mmoja akitokea wilayani Arumeru ambapo ni mjane wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo aliyefariki kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni.
Wahanga hao ambao ni wale walipoteza ndugu zao, waliumizwa maeneo mbalimbali ya mwili na hivyo kupata ulemavu wa kudumu siku ya maandamano na mkutano wa chama hicho wa janiari 5, 2011 ambapo polisi waliwauwa kwa risasi watu watatu Juma Ismail, Denis Shirima na mmoja wa Kenya huku wananchi wengine kadhaa kujeruhiwa.

Wahanga wengine ni wale wa tukio la June 15, mwaka jana ambapo bomu ambalo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alidai lilirushwa na polisi kwenye viwanja vya Soweto wakati akifunga mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata nne za Arusha ambapo walifariki watu watano akiwemo Katibu wa Chadema Kata ya Sokon1, Judith Mollel  ambapo  wengine kadhaa walijeruhiwa.

Aidha wahanga wengine ni wale waliojeruhiwa Juni 18, mwaka jana wakati walipokusanyika kwenye viwanja vya Soweto kwa lengo la kuagaa miili ya wenzao waliuwawa June 15 ambapo polisi waliwatawanya wananchi hao bila kutoa taarifa ya onyo ya kuwataka kutawanyika ambapo viongozi kadhaa wa chama hicho walikamatwa na kufikishwa polisi lakini hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi yao.

0 Comments:

Post a Comment