Friday, May 25, 2012

Arusha Mambo watoa mafunzo ya kuboresha biashara

VIJANA wa kike hapa nchini wametakiwa kutochanganya mahusiano ya kirafiki na kazi au biashara zao ili kuepuka kupoteza wateja hivyo kushindwa kufikia malengo ya kufanikiwa kijiongezea kipato na kuepuka hatari ya kupoteza ajira. Hayo yalisemwa jana Veronica Gerald ambaye ni mshiriki wa mafunzo ya mauzo, masoko na huduma kwa wateja yanayotolewa kampuni ya Arusha Mambo kwenye hoteli ya kitalii ya Arusha Palace. Alisema kuwa hiyo imekuwa ni changamoto kubwa kwa vijana kwani wengi wamekuwa wakitoa huduma kwa kuangalia unadhifu wa mtu au urafiki hivyo kuwahudumia vizuri na kwa haraka jambo ambalo huwa haliwapendezi wateja wengine ambao usubiri muda mrefu kuhudumiwa. “Vijana wa kike wanaweka urafiki mbele kwenye huduma wanaangalia unadhifu wa mtu hii inatakiwa kuepukwa sana kwani inapoteza wateja wale ambao si marafiki zake au nadhifu kwani wanawapa huduma hafifu” alisema Gerald. Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya Arusha mambo, Rosemary Kitosio alisema kuwa mafunzo hayo yanawashirikisha wafanyabiashara wadogo na wakati 18 ambapo yanafanyika kwa awamu sita, kila mwezi yatafanyika siku moja na yanatazamiwa kumalizika mwezi Oktoba mwaka huu. Alisema kuwa mafunzo hayo yanatolewa na mkufunzi, Terry Odiko toka nchini Kenya yanalenga kuwawezesha wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao kitaalam hivyo kujiongezea kipato zaidi kwa kuongeza masoko kutokana na huduma nzuri watakayotoa kwa wateja wao na kujua namna ya kuwapata. Ndesokia alisema kuwa wanaandaa mafunzo mengine juu ya namna ya kuhimili msongo unaotokana na kuzidiwa na majukumu ya kazini na nyumbani ili kuwawezesha watu kufanya kazi zao kwa ufanisi huku wakikaa vizuri na wafanyakazi wenzao na familia zao nyumbani.

No comments:

Post a Comment