Washington/Tehran — Rais wa Marekani, Donald Trump, ameionya Iran dhidi ya kuchukua hatua zozote za kijeshi kuelekea Marekani au washirika wake, akiahidi kutumia “nguvu ambayo haijawahi kuonekana” iwapo vitisho vitatekelezwa.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump aliandika kwa herufi kubwa: “Iran hivi punde imesema kwamba itafanya mashambulizi makali ambayo hayajawahi kuonekana. WASIJARIBU KUFANYA HIVYO KWA SABABU WAKIDHUBUTU, TUTAWAKABILI KWA NGUVU AMBAYO HAIJAWAHI KUONEKANA!”
Kauli hiyo inajiri saa chache baada ya Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) kuonya kuwa itaanzisha operesheni kali za kijeshi dhidi ya maeneo inayoyataja kuwa ni “yanayokaliwa kimabavu” pamoja na vituo vya kijeshi vya Marekani, kulipiza kisasi kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei.
Katika taarifa yake, IRGC ilisema: “Tutaanza operesheni mbaya zaidi katika historia ya vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelekea maeneo yanayokaliwa kimabavu na vituo vya kigaidi vya Marekani muda mfupi ujao.”
Matamshi hayo yameongeza hofu ya kuongezeka kwa mapambano ya moja kwa moja kati ya Iran kwa upande mmoja na Marekani pamoja na Israel kwa upande mwingine, hali inayoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa usalama wa Mashariki ya Kati.
Wakati mvutano ukiendelea, mwana wa shah wa mwisho wa Iran aliyeondolewa madarakani mwaka 1979, Reza Pahlavi, ametoa kauli akiunga mkono kuuawa kwa Khamenei. Katika makala iliyochapishwa na The Washington Post, Pahlavi alimshukuru Trump kwa ujumbe wake kwa watu wa Iran kwamba “wakati wa uhuru wenu imekaribia.”
Pahlavi alidai kuwa kwa karibu nusu karne, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikivuruga utulivu wa majirani zake, kuchochea migogoro kimataifa na kuendeleza mpango wa silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu. Aidha, alitaja kile alichokiita ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Iran, ikiwemo mauaji ya waandamanaji katika misako ya usalama.
Amesema mustakabali wa Iran unapaswa kuhusisha kuandikwa kwa katiba mpya kupitia kura ya maoni na kufuatiwa na uchaguzi huru chini ya uangalizi wa kimataifa.
Ndani ya Iran, mamlaka zimetangaza kuwa rais wa nchi, mkuu wa mahakama na mmoja wa wanasheria wa Guardian Council watasimamia kipindi cha mpito kufuatia kifo cha Khamenei. Wakati huo huo, Assembly of Experts — chombo cha maulama chenye jukumu la kikatiba — kinatarajiwa kukutana haraka iwezekanavyo kumteua Kiongozi Mkuu mpya.
Kwa mujibu wa katiba ya Iran, uteuzi wa kiongozi mpya unapaswa kufanyika bila kuchelewa. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hali ya kiusalama inayotokana na mashambulizi ya kijeshi inaweza kufanya mchakato huo kuwa mgumu zaidi.
Kadri pande husika zinavyoendelea kutoa matamshi makali, jumuiya ya kimataifa inaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo, huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa vita pana zaidi katika eneo ambalo tayari limekumbwa na misukosuko ya muda mrefu.

No comments:
Post a Comment