Wednesday, February 4, 2026

KUELEKEA MAADHIMISHO YA MIAKA 49 YA CCM KUDUMISHA UMOJA,AMANI &MSHIKAMANO

 Na Gift Mongi

Moshi





Katika kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa chama wamefanya ziara  katika Kata ya Kilema Kati, wilaya ya Moshi. 



Tukio hili lilikuwa la kipekee, likiwa na lengo la kuenzi historia ya chama, kuhamasisha umoja wa kitaifa, na kuendelea na juhudi za kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Tanzania.



Mwenyekiti wa Vijana wa CCM wilaya ya Moshi, Chief Yuvenal Raphael Ole Shirima, alitoa wito wa kulinda amani kwa gharama kubwa na kwamba sio kama bidhaa ambayo unaweza kununua dukani


Pia aliwahamasisha vijana wa Tanzania kuendelea kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko na maendeleo ya taifa kwani wao ndio wenye maono ya Tanzania ijayo.


"Amani ni mchakato unaohitaji juhudi za pamoja kwani hatuwezi kupiga hatua mbele kama hatutakuwa na umoja na mshikamano"alisema


Aliongeza " Tunapaswa kutunza na kulinda taifa letu, kwani nchi yetu imejengwa kwa damu, jasho na machozi ya viongozi wetu wa zaman na kama vijana wa CCM, tunawajibika kuhakikisha kuwa amani inaendelea kutawala," alisema Shirima mbele ya wanachama na wananchi wa Kata ya Kilema Kati.



Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Ramadhan Mahanyu, alieleza umuhimu wa umoja na mshikamano na  umuhimu wa kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia maendeleo ya kweli.


 Akiongea mbele ya   wanachama wa CCM na wananchi wa Kata ya Kilema Kati, alikumbusha kwamba mafanikio ya chama cha Mapinduzi yamejengwa juu ya msingi wa umoja na mshikamano.


"Chama chetu cha Mapinduzi kimefika hapa leo kwa sababu ya juhudi za pamoja. Bila umoja na mshikamano, hakuna maendeleo ya kudumu yanayoweza kupatikana"alisema


"Nawaenzi viongozi wetu waasisi kwa ujasiri wao na kwa kujitolea kwao, kwani CCM ni chama cha watu wa amani, na tuna wajibu wa kulinda amani ya taifa letu," 



No comments:

Post a Comment