Dar es Salaam, Agosti 12, 2025 — WALIOWAHI kuwa waandishi wa habari wa muda mrefu nchini, Salum Mwalimu na Devotha Minja, leo wamechukua rasmi fomu za uteuzi wa kugombea nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma). Zoezi hilo limefanyika katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jijini Dar es Salaam.
Salum Mwalimu, aliyewahi kuwa mtangazaji na mwandishi wa habari katika televisheni ya Channel Ten, kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Chaumma, nafasi ya juu inayoongoza shughuli za kila siku za chama kitaifa. Devotha Minja, aliyewahi kuwa mwandishi wa ITV mkoani Morogoro, ni Makamu Mwenyekiti wa Chaumma upande wa Tanzania Bara, nafasi inayompa mamlaka ya kisera na kiutendaji katika mikoa yote ya bara.
Wagombea hao walikabidhiwa mkoba wa fomu za uteuzi na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, ikiwa ni hatua rasmi kuelekea uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais, unaotarajiwa kufanyika Agosti 27, 2025.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi, kampeni rasmi za uchaguzi mkuu zitaanza mara baada ya uteuzi wa wagombea, huku uchaguzi mkuu ukipangwa kufanyika Oktoba 28, 2025. INEC imeendelea kusisitiza umuhimu wa amani, utii wa sheria, na usawa kwa wagombea wote.
Kwa sasa, vyama vya siasa vinaendelea na mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za uteuzi kwa nafasi mbalimbali za kisiasa, ikiwemo Urais, Ubunge na Udiwani. Wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huo kwa amani na kwa kufuata sheria.



0 Comments:
Post a Comment