Wamasai Msomera Washiriki Tamasha la Kitamaduni Kilimanjaro



Na Mwandishi Wetu, Sanya Juu – Kilimanjaro

Jamii ya Wamasai waliotoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wameshiriki kikamilifu Tamasha la Kitamaduni na Kimila la Wamasai Orkwaak le Maasae 2025, linalofanyika katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.



Tamasha hilo limekusanya zaidi ya watu 30,000 kutoka jamii ya Kimasai nchini na mataifa jirani, likiwa na lengo la kudumisha, kuenzi na kuendeleza mila, desturi na utambulisho wa kitamaduni wa jamii hiyo. Pia linaweka jukwaa la kubadilishana maarifa na kuonesha utajiri wa urithi wa kitamaduni wa makabila ya Tanzania.



Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa tamasha hilo, mmoja wa wakazi wa Msomera, Juliana Thadei Saidimu, amesema:
"Tuna furaha kubwa kuwa sehemu ya tukio hili. Tumekutana na wenzetu kutoka maeneo mbalimbali na hata mataifa mengine kusherehekea utamaduni wetu. Hili ni jambo la kujivunia."


Kiongozi wa kimila kutoka Msomera, Komba Riko Lodoo, amesema hatua ya serikali kuendelea kushirikisha jamii hiyo katika shughuli za kijamii na kitamaduni inaonesha kuwa, licha ya kuondoka Ngorongoro, bado wameendelea kuwa thabiti katika kuhifadhi mila na utambulisho wao.

"Wananchi tuliotoka Ngorongoro kwenda Msomera si tu kwamba tumekuwa huru kiuchumi na kijamii, bali pia tuna uhuru wa kufanya shughuli zetu za kimila kwa kuwa tuna maeneo ya wazi. Tunapata fursa adhimu kama hii ya kushiriki na wenzetu katika kudumisha mila zetu kwa pamoja," amesema Laigwanan Lodoo.



Tamasha hilo la siku tatu limekuwa sehemu muhimu ya juhudi za jamii ya Wamasai kulinda, kuhifadhi na kukuza urithi wa kitamaduni, kwa lengo la kuhakikisha kuwa mila na desturi zao zinabaki kuwa urithi hai kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

0 Comments:

Post a Comment